Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua rasmi dirisha la Awamu ya Nne ya Tuzo kwa watafiti na wahadhiri wanaochapisha matokeo ya tafiti katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 18, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Juni 19 hadi Oktoba 31, 2026, likilenga kutoa fursa kwa watafiti kuwasilisha machapisho yao kwa ajili ya ushindani wa tuzo hizo.
Amesema tuzo hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuhamasisha utafiti na ubunifu wa ndani, kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje, pamoja na kuimarisha mchango wa sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, serikali imetenga Shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa tuzo hiyo, ikiwa ni motisha kwa watafiti kufanya tafiti zenye ubora na zinazotoa suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi.
Prof. Mkenda amebainisha kuwa majarida yenye hadhi ya juu hutambulika kimataifa na hutoa nafasi kwa watafiti kupata uhalali na heshima katika jamii ya kisayansi duniani.
Ameongeza kuwa katika awamu zilizopita, jumla ya machapisho 336 yaliingia katika ushindani, ambapo machapisho 86 yalitunukiwa, huku watafiti 200 wakinufaika na tuzo hizo kutokana na mchango wao wa tafiti zilizochapishwa.
Amesema tuzo hiyo hutolewa katika nyanja nne ambazo ni Sayansi Asilia na Hisabati, Afya na Sayansi Shirikishi, Sayansi za Wanyama na Kilimo, pamoja na Uhandisi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika utafiti na ubunifu ili kuongeza uzalishaji wa maarifa, kuimarisha teknolojia, na kuongeza ushindani wa taifa katika uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa.
