Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu ya usafiri inayolenga kuimarisha huduma za usafirishaji katika Ushoroba wa Kati (Central Corridor), huku mafanikio makubwa yakionekana katika reli ya kisasa ya SGR, Bandari ya Dar es Salaam na usafiri wa majini.
Akizungumza katika Mkutano wa 15 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Ushoroba wa Kati (ICM) unaofanyika Dar es Salaam leo Juni 18, 2026, Prof. Mbarawa amesema ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Kigoma pamoja na Uvinza hadi Musongati nchini Burundi utaongeza kwa kiasi kikubwa muunganiko wa kikanda, biashara na ushirikiano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema tangu kuanza kwa huduma za usafiri wa abiria wa SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma mwezi Juni 2024, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanikiwa kusafirisha zaidi ya abiria milioni sita.
Kwa sasa, safari nane hufanyika kila siku kati ya Dar es Salaam na Dodoma, huku safari tatu zikifanyika kati ya Dar es Salaam na Morogoro, zikisafirisha wastani wa abiria kati ya 8,000 na 11,000 kwa siku.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa SGR imekuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya usafiri nchini Tanzania kwa kuwavutia wananchi wengi kutumia reli badala ya usafiri wa barabara na anga.
Aidha, amesema TRC ilianza rasmi huduma za usafirishaji mizigo kupitia SGR mwezi Juni 2025 kutoka Dar es Salaam hadi Ihumwa mkoani Dodoma.
Pia, shirika hilo liko katika hatua za mwisho za ujenzi wa kituo cha kubadilishia mizigo cha Bahi, ambacho kitaiwezesha mizigo kuhamishwa kwa urahisi kutoka reli ya kisasa kwenda reli ya zamani kwa usafirishaji kuelekea Isaka na maeneo mengine.
Kuhusu Reli ya TAZARA, Prof. Mbarawa amesema Tanzania na Zambia zilitia saini makubaliano mwezi Septemba 2025 ya kuikabidhi reli hiyo kwa mwekezaji kutoka China kwa mfumo wa ubia, hatua inayotarajiwa kuifufua reli hiyo kupitia ukarabati mkubwa wa miundombinu na ununuzi wa vichwa na mabehewa mapya.
Katika sekta ya bandari, Waziri huyo amesema ushirikishwaji wa kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Limited katika usimamizi wa shughuli za makontena umeongeza ufanisi mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa hadi Machi 2026, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imehudumia tani milioni 29.66 za mizigo ikilinganishwa na tani milioni 23.18 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 27.96.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa uhamishaji mizigo kutoka bandarini kwa kuendeleza bandari kavu katika maeneo ya Kwala, Morogoro, Ihumwa, Isaka, Fela na Katosho ili kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.
Katika usafiri wa majini, Prof. Mbarawa amesema Serikali inaendelea na ukarabati wa meli za MV Mwongozo na MV Liemba katika Ziwa Tanganyika pamoja na ujenzi wa karakana ya kisasa ya meli na meli mpya ya mizigo aina ya Roll-on/Roll-off (Ro-Ro).
Kwa upande wa Ziwa Victoria, amesema Serikali inaendelea na ukarabati wa meli za MV Nyangumi na MV Clarias pamoja na ujenzi wa meli mpya ya MV New Mwanza na meli nyingine ya Ro-Ro kwa lengo la kuimarisha huduma za usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ufanisi wa usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji katika Ushoroba wa Kati ili kuongeza biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi wanachama.

