Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah akisalimiana na Bi. Salama Salehe Ghulum (Mama Salehe) na Bi. Rafran Ismail Khan ambao walikuwa majirani zake wakati akiishi Magomeni Mikumi Jijini Dar es Salaam katika miaka ya 1980s. Mhe. Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah alikutana na jirani yake huyo wa siku nyingi katika hafla ya chakula cha jioni alichoandaliwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Mei, 2025. (Picha na Ikulu)
…………
Ziara ya Rais wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania kuanzia Juni 19 hadi 21, 2026, ni tukio la kihistoria, kisiasa na kiuchumi linalobeba kumbukumbu za harakati za ukombozi wa Afrika na wakati huo huo kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa haya mawili rafiki.
Kwa Netumbo Nandi-Ndaitwah, Tanzania si taifa la kawaida katika historia yake. Ni nchi iliyokuwa sehemu ya maisha yake wakati wa harakati za ukombozi wa Namibia kupitia chama cha SWAPO (South West Africa People’s Organisation), kilichoongoza mapambano ya kuikomboa Namibia kutoka katika utawala wa kikoloni wa Afrika Kusini.
Mwaka 1980 hadi 1986, Netumbo alikuwa mwakilishi mkuu wa SWAPO katika Ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na makao yake Dar es Salaam. Katika kipindi hicho aliishi eneo la Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, ambako alijenga mahusiano ya karibu na Watanzania waliokuwa majirani zake wakati wa maisha yake ya uhamishoni na harakati za ukombozi.
Historia hiyo ndiyo inayofanya ziara yake ya sasa kuwa na maana ya kipekee. Mbali na shughuli rasmi za kiserikali, ziara hiyo inamrudisha katika sehemu ya historia yake binafsi na ya kisiasa, katika taifa ambalo lilitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Namibia na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika.
Katika ziara yake ya kwanza akiwa Rais wa Namibia, Netumbo alipata fursa ya kukutana tena na baadhi ya majirani zake wa zamani wa Magomeni, akiwemo Bi. Salama Salehe Ghulum (Mama Salehe) na Bi. Rafran Ismail Khan. Mkutano huo uliibua kumbukumbu za miaka ya mapambano ya uhuru na kuonesha namna Tanzania ilivyobaki kuwa sehemu muhimu ya maisha yake hata baada ya kupita zaidi ya miongo minne.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkaribisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Mei, 2025.
Katika ziara yake ya pili nchini ambayo anakuja kwa Mwaliko wa Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, anakuja Tanzania ikiwa ni mara ya pili , Netumbo anatarajiwa kutembelea tena eneo la Magomeni alikowahi kuishi. Hivyo, ziara hii si tu ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia, bali pia ni safari ya kurejea katika sehemu ya historia yake binafsi iliyomshuhudia akiwa mwanaharakati wa ukombozi mpaka kuwa Mkuu wa nchi.
Kwa Namibia, Tanzania haikuwa tu mshirika wa kidiplomasia bali ilikuwa ngome muhimu ya harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilitoa hifadhi, mafunzo na msaada wa kisiasa kwa wapigania uhuru wa Namibia kupitia SWAPO pamoja na harakati nyingine za ukombozi katika ukanda huo.
Kutoka Magomeni hadi Ikulu ya Windhoek, simulizi ya Netumbo inaakisi safari ya kizazi cha viongozi wa Afrika waliopitia mapambano ya uhuru na baadaye kubeba dhamana ya kuongoza mataifa yao katika kipindi cha maendeleo, mageuzi ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda.
Ziara hiyo pia inafanyika wakati Tanzania inaongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kiongozi ambaye ameendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kufungua fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kukuza maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.
Kwa upande mwingine, tangu alipoingia madarakani mwaka 2025, Netumbo ametekeleza mageuzi mbalimbali yanayolenga kuongeza ufanisi wa serikali yake, kuimarisha uwajibikaji, kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Namibia.
Kutokana na mwelekeo huo, mkutano kati ya Dkt. Samia na Dkt. Netumbo unawakutanisha viongozi wawili wenye maono yanayofanana kuhusu matumizi bora ya rasilimali za taifa, kuimarisha uchumi, kuvutia uwekezaji na kuongeza nafasi ya Afrika katika ushindani wa kimataifa.
Muhimu zaidi, ziara hiyo inawakutanisha wanawake wawili waliofikia nafasi za juu kabisa za uongozi katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika. Hili ni jambo lenye uzito wa kisiasa na kijamii kwa bara ambalo kwa muda mrefu nafasi za juu za uongozi zimekuwa zikitawaliwa zaidi na wanaume.
Miongoni mwa maeneo muhimu yanayotarajiwa kujadiliwa na viongozi hao ni biashara, uwekezaji, madini, nishati, utalii, kilimo, miundombinu na maendeleo ya sekta binafsi. Haya ni maeneo yanayoendelea kuwa nguzo muhimu za ukuaji wa uchumi wa Tanzania na Namibia.
Katika sekta ya madini, Namibia imejijengea sifa katika usimamizi wa sekta ya almasi huku Tanzania ikiwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika.
Ushirikiano katika eneo hili unaweza kusaidia kuongeza thamani ya rasilimali hizo ndani ya nchi kabla ya kuzipeleka katika masoko ya kimataifa.
Katika sekta ya nishati, Namibia imeendelea kuvutia dunia kutokana na fursa za mafuta, gesi na nishati safi hususan Green Hydrogen, wakati Tanzania imejijengea uzoefu mkubwa katika usimamizi wa gesi asilia. Kubadilishana uzoefu wa kisera, kisheria na kitaalamu kunaweza kuwa moja ya matokeo muhimu ya mazungumzo hayo.
Viongozi hao pia wanatarajiwa kujadili namna ya kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kuongeza biashara ya ndani ya bara. Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inaweza kupanua zaidi masoko ya bidhaa zake katika Kusini mwa Afrika huku Namibia ikitumia Tanzania kama lango muhimu kuelekea soko la Afrika Mashariki.
Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Walvis Bay zinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha biashara kati ya Mashariki na Kusini mwa Afrika. Ushirikiano katika sekta ya usafirishaji na miundombinu unaweza kuongeza ushindani wa bidhaa za nchi hizo mbili katika soko la bara na la kimataifa.
Baada ya mazungumzo yao rasmi, Samia na Netumbo wanatarajiwa kuzungumza na wanahabari kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa na mwelekeo mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Kauli zao zitatoa taswira ya namna urafiki wa kihistoria wa Tanzania na Namibia unavyotafsiriwa katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia.
Kwa ujumla, ziara ya Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania ni zaidi ya ratiba ya kawaida ya kidiplomasia. Ni safari inayounganisha historia ya ukombozi wa Afrika, kumbukumbu za Magomeni, mageuzi ya kisasa ya kiuchumi na maono ya viongozi wawili wanawake wanaoongoza mataifa yao katika kipindi muhimu cha maendeleo.
Iwapo mazungumzo yao yatazaa mikakati mipya ya ushirikiano, basi ziara hii inaweza kukumbukwa kama hatua muhimu iliyounganisha urithi wa ukombozi na fursa za uchumi wa kisasa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Namibia.
