Afisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bi. Anne Swila, akitoa elimu kwa wananchi kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, walipotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Msimamizi wa Fedha Mkuu, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Grace Samwel, akitoa elimu kwa mwananchi kuhusuusimamizi wa fedha binafsi, walipotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Mchumi Mkuu wa Idara ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Wizara ya Fedha, Bi. Josephina Buhili, na Mchumi Daraja la Kwanza wa Idara ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Bi. Anastazia Amandi, wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu, majukumu, mipango na malengo pia miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Idara hiyo, walipotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Mchumi Mwandamizi wa Idara ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Bi. Consolatha Komba, akifafanua kwa wananchi kuhusu, vipaumbele na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, walipotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Maafisa wa Wizara ya Fedha wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kuhusu majukumu yanayotekelezwa na wizara, wakati wananchi hao walipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yenye kauli mbiu ‘Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Maendeleo Endelevu’, yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma.)

……….

Na. Jordan Mbwambo, WF, Dodoma.

Serikali imeanza kutumia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, hatua inayolenga kufungamanisha na kuboresha usimamizi wa shughuli za Mnyororo wa Ugavi nchini ili kuongeza ufanisi, matumizi bora ya rasilimali na kupata thamani halisi ya fedha za umma.

Hayo yalibainishwa na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Usimamizi wa Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bi. Anne Swila, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Maonesho la Wizara ya Fedha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yenye Kaulimbiu ya “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Alisema kuwa Sera hiyo inalenga maeneo sita makuu, yakiwemo Ununuzi wa Umma, Ugomboaji na Uondoshaji wa Mizigo ya Serikali, Upokeaji na Urejeshaji, Utunzaji na Uhifadhi, Usambazaji, pamoja na uhifadhi wa Mazingira na Utawala Bora.

‘‘Kwa miaka mingi tumekuwa na sheria nzuri za ununuzi, lakini hazikuwa zimeunganishwa kwa msingi mmoja wa kisera, Sera hii sasa inakwenda kuziba pengo hilo na kuhakikisha kila shilingi ya umma inatumika kwa thamani yake halisi, kwa kuhakikisha mikakati ya utekelezaji inajumuisha kuimarisha udhibiti wa bei, uchaguzi wa wazabuni, na kuendeleza Kada ya Ununuzi na Ugavi Serikalini ” alieleza Bi. Swila.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa Sera hii itaongeza ushindani na kuwapa fursa wazabuni wazawa, sekta binafsi na makundi maalum ya kijamii, hatua itakayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi na kuchochea ukuaji wa ajira.

Bi. Swila alisema Sera hiyo pia inatarajiwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki na rasilimali za ndani, kuvutia uwekezaji katika miundombinu ya uhifadhi na usambazaji, na hivyo kuifanya sekta ya mnyororo wa ugavi kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

‘‘Miongoni mwa mafanikio yanayotarajiwa ni kuongezeka kwa ufanisi, udhibiti bora wa gharama, kuimarika kwa ubora wa huduma kwa wananchi, ongezeko la ajira, uzingatiaji wa uhifadhi wa mazingira, na kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini utakaohakikisha utekelezaji wa sera unaleta tija iliyokusudiwa’’, alifafanua Bi Swila.

Aidha, alisema kuwa Sera hiyo itawezesha kuwepo kwa mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini, hatua itakayoifanya sekta ya mnyororo wa ugavi kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuchangia kupunguza umasikini nchini.

Sera hiyo inatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2026 hadi 2036 na tathmini ya utekelezaji itafanyika kila baada ya miaka mitano ya utekelezaji.