Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 19 Juni, 2026 kwa ziara ya kitaifa.

Ziara hiyo, ambayo ni ya pili kuifanya nchini Tanzania tangu aingie madarakani, inaendelea kudhihirisha uhusiano wa kindugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Namibia, uliojengwa katika misingi ya harakati za ukombozi wa Afrika, mshikamano na ushirikiano wa maendeleo unaonufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Tarehe 20 Juni, 2026, Rais Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, yatakayojikita katika masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa katika maeneo yenye maslahi ya pamoja. Baadaye, viongozi hao wawili watazungumza na waandishi wa habari.

Akiwa nchini, Rais Nandi-Ndaitwah atatembelea eneo la Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam, ambako aliwahi kuishi katika miaka ya 1980 alipokuwa Mwakilishi Mkuu wa chama cha South West Africa People’s Organization (SWAPO), hatua inayobeba kumbukumbu muhimu za mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Namibia.

Vilevile, atatembelea Kambi ya Wapigania Uhuru wa Harakati za Ukombozi Barani Afrika iliyopo Kongwa, mkoani Dodoma.

Rais Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kuhitimisha ziara yake nchini tarehe 22 Juni, 2026.