Magari saba (07) yaliyobainika kuwa na ubovu mkubwa yameondolewa namba za usajili, mengine yakatozwa faini huku baadhi yakielekezwa kurekebisha kasoro mbalimbali za kiufundi, kufuatia operesheni maalumu ya ukaguzi wa magari yanayotoa huduma za usafiri wa abiria iliyofanywa na Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe katika Wilaya ya Songwe na vijiji vyake, kwa lengo la kuimarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Akizungumza Juni 16, 2026 wakati wa operesheni hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Joseph Bukombe alisema operesheni hiyo, itakayoendelea hadi mwisho wa mwezi Juni, inalenga kuhakikisha magari yote yanayosafirisha abiria yanazingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kulinda maisha ya wananchi na kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.
ACP Bukombe alisema ukaguzi uliofanyika umebaini baadhi ya magari kubeba abiria kupita kiwango kilichoruhusiwa, kutumia matairi yaliyochakaa, pamoja na kuwa na hitilafu katika mifumo ya usalama ikiwemo spring na shock absorber, ikiwa baadhi ya madereva walikutwa wakiendesha vyombo vya moto wakiwa na leseni zilizoisha muda wake, jambo ambalo ni kinyume na sheria za usalama barabarani.
Katika hatua nyingine, ACP Bukombe alisema operesheni hiyo imebaini baadhi ya wasafirishaji kutowapatia abiria tiketi za kielektroniki kama inavyotakiwa kisheria na badala yake kutoa tiketi za kawaida, hali inayochangia upotevu wa mapato ya Serikali na kuwanyima abiria haki na stahiki zao.
Mwisho, ACP Bukombe amesisitiza kuwa operesheni hiyo itaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha huduma za usafiri vijijini zinatolewa kwa kuzingatia sheria, usalama na maslahi ya wananchi.

