TAWLA imeitaka Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya sheria zinazohusiana na ndoa za utotoni, ikieleza kuwa bado kuna vipengele vinavyokwamisha jitihada za kulinda haki na ustawi wa mtoto wa kike nchini.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma katika kikao kati ya TAWLA na wabunge kilicholenga kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike, hususan suala la ndoa za mapema zinazoathiri elimu na maendeleo yao ya baadaye.
Akizungumza katika kikao hicho, mwakilishi wa TAWLA, Tike Mwambipile, amesema ndoa za utotoni zimeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa watoto wa kike kwa kuwakatisha masomo na kuwanyima nafasi ya kufikia malengo yao ya maisha. Amesisitiza kuwa mtoto wa kike anapaswa kupewa muda wa kujifunza, kukua na kujijenga kabla ya kuingia katika majukumu ya ndoa.
Kwa upande wao, wabunge walikubaliana na hoja hiyo na kueleza kuwa kuna umuhimu wa kupitia upya baadhi ya sheria ili ziendane na mabadiliko ya kijamii pamoja na malengo ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Mbunge wa Kasulu Mjini na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wabunge Tanzania (TWPG), Joyce Ndalichako amesema mtoto wa umri mdogo, ikiwemo miaka 14, anapaswa kuwa shuleni badala ya kuozeshwa, akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya elimu unapaswa kulindwa kwa kuhakikisha watoto wote wanamaliza masomo yao.
Ameongeza kuwa mchakato wa maboresho ya sheria unapaswa kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayosisitiza usawa wa kijinsia na ustawi wa wananchi wote.
Kwa ujumla, pande zote zimekubaliana kuwa ushirikiano kati ya serikali, wabunge na wadau wa maendeleo ni muhimu ili kuimarisha ulinzi wa mtoto wa kike na hatimaye kutokomeza kabisa ndoa za utotoni nchini.

