Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amezindua Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) pamoja na transfoma ya kudhibiti umeme kilichopo Mbande, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.Akizungumza Juni 16, 2026 katika uzinduzi huo, Waziri Ndejembi amesema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza ufanisi wa mfumo wa usambazaji na kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi katika maeneo ya Kongwa na wilaya jirani.

Aidha, amebainisha kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaimarisha huduma ya umeme katika wilaya za Kongwa, Gairo, Chamwino na baadhi ya maeneo ya wilaya za Mpwapwa na Kiteto.Pia amesema kuwa miundombinu hiyo itaongeza uthabiti wa mfumo wa usambazaji umeme, kupunguza athari za hitilafu, kuboresha viwango vya umeme na kuongeza uwezo wa TANESCO kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi na wawekezaji.Ameongeza kuwa Serikali inatarajia kuona ongezeko la shughuli za uzalishaji mali, kuimarika kwa biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma za jamii kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika. Aidha, amesisitiza kuwa hatarajii baada ya mradi huo mkubwa kukamilika bado kuwepo changamoto za kuunganisha umeme kwa wananchi.

Pia amebainisha kuwa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uthabiti wa mfumo wa usambazaji umeme na kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi. Amesema kwa muda mrefu wananchi wa Kongwa walitegemea umeme wa njia moja wa msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za mara kwa mara za upatikanaji wa umeme.

Aidha, amesema kukamilika kwa mradi huo kunahakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika wenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya megawati 130. Serikali pia imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 514 katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere kupitia Chalinze hadi Dodoma kwa msongo wa kilovoti 400.Awali akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema kuwa ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 92 kutoka Zuzu hadi Mbande Kongwa, pamoja na ujenzi wa kituo cha kubadilisha njia za usambazaji umeme na kifaa cha AVR, umekamilika.

Amesema kifaa hicho kina kazi ya kurekebisha viwango vya umeme pale vinapokuwa juu au chini ya kiwango kinachotakiwa, ili kuhakikisha wateja wanapata umeme wa uhakika na wenye ubora.

Pia ameongeza kuwa mradi huo umekamilika na sasa upo katika kipindi cha uangalizi, huku akibainisha kuwa changamoto zilizokuwa zikiathiri upatikanaji wa huduma ya umeme zimepungua kwa zaidi ya asilimia 90.