Na Shaban K. Juma, Dar es Salaam
Serikali imewataka wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa hiari na mara kwa mara ili kuhakikisha upatikanaji wa damu salama na ya kutosha kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji nchini.
Wito huo umetolewa leo Juni 14, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Damu ni tiba ya kipekee ambayo haiwezi kutengenezwa kiwandani. Wagonjwa wanaopoteza damu kutokana na ajali, akina mama wakati wa kujifungua, watoto wenye malaria kali, wagonjwa wa saratani pamoja na sikoseli hutegemea moyo wa kujitolea wa wachangia damu,” amesema Dkt. Samizi.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachangia damu katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, watoto wenye upungufu wa damu pamoja na wagonjwa wa saratani na sikoseli, ndiyo maana imeendelea kuwaenzi na kuwapongeza kwa mchango wao wa kuokoa maisha.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha damu inayopatikana inatumika kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya damu hospitalini na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya damu ikiwemo chembe nyekundu, chembe nyeupe, sahani damu (platelets) na plasma.
Dkt. Samizi, Serikali inaendelea kuimarisha na kuongeza vituo vya damu salama katika mikoa yote nchini sambamba na kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutengeneza na kuhifadhi mazao ya damu ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa usalama wakati wote.
Pia amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu na kuondoa hofu zinazohusiana na uchangiaji damu kwa lengo la kuongeza akiba ya damu salama nchini.

