Na Abdu Madenge, WAF – Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amewataka wataalamu wa afya nchini kuendelea kushirikiana, kupeana nguvu na kubadilishana uzoefu ili kudumisha na kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya, hususan katika eneo la afya ya uzazi, mama na mtoto.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo tarehe 13 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Kikao cha Kamati ya Kitaalam (TWG 5) ya Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ambapo alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito. Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio hayo yanaweza kupotea iwapo mshikamano, juhudi na afua zinazotekelezwa hazitasimamiwa ipasavyo.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Mohammed Makuwani, amesema kuwa kikao hicho kimeandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa lengo la kupitia utekelezaji wa afua mbalimbali za afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na kujadili mafanikio, changamoto na vipaumbele vya utekelezaji katika ngazi zote za huduma.

Dkt. Makuwani amesema kuwa tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Serikali imeendelea kuimarisha uwekezaji katika afya ya uzazi, mama na mtoto kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma, upatikanaji wa vifaa tiba, ongezeko la wataalamu wa afya pamoja na kuimarishwa kwa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga, hatua ambazo zimechangia kupatikana kwa mafanikio makubwa yanayoonekana sasa.

Alisema pamoja na uwepo wa wadau wanaochangia rasilimali za kifedha, wataalamu wa ndani wana wajibu mkubwa wa kusaidiana kwa kubadilishana utaalamu wa kiufundi na kujitolea kwa dhati ili kulinda mafanikio yaliyofikiwa.

“Haipendezi kuona Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akipata utambuzi mkubwa wa kimataifa halafu baadaye nchi yetu ikaonekana imerudi nyuma. Tunapaswa kuhakikisha tunaendelea kusaidiana na kuimarishana ili mafanikio haya yaendelee kudumu,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesema jitihada zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wataalamu wa afya nchini hazilengi Tanzania pekee, bali zinapaswa kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi nyingine za Afrika kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuboresha afya ya uzazi.