Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Waziri wa Maji kwenda Mkoa wa Mwanza kushughulikia mara moja changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi wa mkoa huo na kuhakikisha huduma hiyo inarejea kwa haraka.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo, Jumapili Juni 14, 2026, wakati akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Kiomboi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Lulumba, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Amesema amepokea taarifa kuhusu changamoto ya maji katika Mkoa wa Mwanza na tayari amemuelekeza Waziri mwenye dhamana ya maji kwenda eneo husika kusimamia upatikanaji wa suluhisho la haraka.
“Nimemtuma Waziri aende haraka Mwanza akasimamie jambo lile mpaka maji yapatikane. Sisi watu wa Singida tunataka tupate maji toka Mwanza. Simiyu tunataka tupate maji toka Mwanza. Dodoma tunataka tupate maji toka Mwanza. Tabora, wengine wameshaanza kupata maji toka Mwanza. Leo kuja kuambiwa Mwanza, pale pale lilipo Ziwa Victoria, pana shida ya maji. Hili ni jambo ambalo haliwezi kueleweka, na wala hatuwezi kulielewa,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo wakati chanzo cha maji kinajulikana na miundombinu ya mradi ipo.
“Hatutaki ngonjera za maneno. Hawa wanasema si bomba limekuwaje, hawa wanasema si umeme umekuwaje. Chanzo sisi tunajua kiko pale, hatuna shida ya chanzo cha maji, na mradi upo, na maji yapo. Haya mambo mengine ni ya ngonjera, mimi sitaki kuyasikia,” amesema.
Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa sekta ya maji pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa haraka.
“Mkuu wa Mkoa awatafute wataalamu wake, awatafute TANESCO na wataalamu wa maji. Wachimbe kiini cha tatizo na wakeshe mpaka wananchi wapate maji. Kunapopambazuka kesho nipate majawabu kwamba maji yamepatikana,” amesema.
Juni 9, 2026, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu upungufu wa huduma ya maji uliosababishwa na hitilafu za umeme zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Wakati huohuo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji katika Tarafa ya Kiomboi na maeneo mengine ya Wilaya ya Iramba inapata ufumbuzi wa kudumu kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta hiyo nchini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele maalum katika sekta ya maji kwa kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
“Niwahakikishie kwamba hili ni eneo ambalo Mheshimiwa Rais ameliwekea kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu maji ni uhai, maji ni maisha. Tulihangaika kupata chanzo cha uhakika cha maji na sasa kimepatikana, hatua mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji pamoja na kuimarisha uwezo wa uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabwawa na upimaji wa vyanzo vya maji ili kukabiliana na changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi amesema Serikali inaendelea na usanifu wa barabara ya Kiomboi–Kisiriri–Sibiti kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami na kuboresha mawasiliano kati ya wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani.
Aidha, amesema usanifu wa barabara ya Kitusha–Galangala–Kisana–Kinampanda–Kisiriri umekamilika, huku Serikali ikiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi mingine ya barabara katika Wilaya ya Iramba ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Pia amesema usanifu wa daraja la kuunganisha eneo la Hospitali ya Kiomboi na maeneo ya Meli pamoja na Iguguno umekamilika na hatua zinazofuata ni kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo.
Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Chuo Kikuu katika eneo la Kiomboi baada ya eneo lililotengwa kuridhiwa na wataalamu husika.
“Hapa Kiomboi tutakuwa na Chuo Kikuu. Eneo limekaguliwa na kuridhiwa na hatua za utekelezaji zinaanza,” amesema.
Amesema pindi ujenzi wake utakapokamilika, Chuo Kikuu hicho kinatarajiwa kuanza kwa awamu ya kwanza kwa uwezo wa kuhudumia wanafunzi takribani 10,000.

