Na. Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imezindua mradi wa Kituo cha Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme katika Ofisi za TANESCO jijini Dodoma,  Juni 11, 2026.

Uzinduzi huo umefanyika katika Makao Makuu ya TANESCO jijini Dodoma, ukiongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi. Hafla hiyo pia imeambatana na utiaji saini na uzinduzi wa miradi ya nishati safi ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Kuchajia Vyombo vya Usafiri Vinavyotumia Umeme (EV Charging Stations) pamoja na Mpango wa Ukopeshaji wa Majiko ya Umeme kwa Wateja wa TANESCO (On-Bill Financing – OBF).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Ndejembi amesema kuwa Serikali haitaki kusimama kwenye uzinduzi pekee bali kuongoza kwa mfano katika matumizi ya nishati safi. Amesema kuwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kuhakikisha Mji wa Serikali Mtumba unaweka miundombinu ya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.

Aidha, amesema kuwa Wizara ya Nishati inapaswa kuwa kinara kwa kuanza kuagiza magari ya umeme au mseto (hybrid) katika mwaka wa fedha 2026/27, huku akiitaka TANESCO kuanza kutumia magari yanayotumia umeme katika shughuli zake za kila siku.

Pia amesema kuwa dunia inaelekea katika uchumi wa kijani na kwamba Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeamua kwenda sambamba na mabadiliko hayo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa mafuta.

Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yalikuwa asilimia sita mwaka 2021 na sasa yamefikia asilimia 24, huku lengo likiwa kufikia asilimia 80. Amesema kuwa mafanikio hayo yanaonyesha kuwa inawezekana pia kufikia lengo la kuwa na angalau asilimia 20 ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme au teknolojia ya hybrid nchini.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amebainisha kuwa TANESCO kwa kushirikiana na UDP itajenga vituo 50 vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme nchini, vikiwemo magari na bajaji.

Aidha, amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unatokana na maelekezo na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

 

Pia amebainisha kuwa ifikapo mwaka 2034, lengo ni kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, huku sekta ndogo ya umeme ikipewa jukumu la kuchangia asilimia 20 ya lengo hilo. Amesema kuwa kwa sasa mchango huo umefikia asilimia 4.8.

Ameongeza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali umeiwezesha TANESCO kuwa na zaidi ya megawati 4,000 za umeme, huku akibainisha kuwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5 una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Aidha, amebainisha kuwa TANESCO kwa sasa ina wateja takriban milioni sita na inatarajia kufikia milioni 6.5, huku makubaliano yaliyosainiwa yakilenga kuwakopesha majiko ya umeme wateja milioni moja ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Pia amesema kuwa vigezo vya kupata mkopo wa jiko la umeme ni kuwa mteja wa TANESCO kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu na kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA), huku awamu ya kwanza ikiwalenga wamiliki wa kaya.

Ameongeza kuwa uzoefu wa mradi wa MECS uliowahusisha wateja zaidi ya 1,000 umeonyesha mafanikio makubwa, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wanufaika waliweza kulipa madeni yao, hali iliyowapa imani ya kupanua mpango huo kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuwafikia wateja milioni moja nchini.