Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji amekabidhi kwa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA Tuzo ya Mafanikio katika Utoaji wa Huduma bora Mwaka 2026 (Quality Achievement Award 2026) pamoja na Cheti cha Ushindi wa Pili (First Runner-Up) katika Tuzo za Ubora wa Taifa 2025/2026 kwenye kikao cha bodi hiyo kinachoendelea leo Juni 11, 2026 jijini Dar es salaam.
Tuzo ya “Quality Achievement Award 2026” ilitolewa tarehe 31 Mei 2026 jijini Brussels, Ubelgiji na Taasisi ya “European Society for Quality Research (ESQR)” huku Cheti cha Ushindi katika Tuzo za Ubora wa Taifa 2025/2026 kilitolewa na Shirika la Viwango Tanzania kwa kutambua taasisi zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma na kuzingatia viwango vya ubora, kilitolewa juni 05, 2026 jijini Dar es salaam.
Bodi ya Wadhamini TANAPA inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jenerali George Waitara, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, imepokea tuzo hizo na kuipongeza Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Maafisa na Askari Uhifadhi kwa kuendelea kutambulika kimataifa na kitaifa katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya TANAPA ya uhifadhi na maendeleo ya utalii nchini.
Vilevile, Bodi ya Wadhamini imetoa wito kwa watumishi wote wa Shirika kuhakikisha kuwa kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu ili kuendelea kufanikisha malengo ya Shirika na Taifa kwa ujumla pamoja na kupata tuzo nyingi zaidi.

