Meneja wa Moyo Tented Camps inayomilikiwa na kampuni ya Conservation Caravan Safaris, Mary Loishooki akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
……………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Wakati juhudi za kuitangaza Tanzania kama moja ya destinisheni bora za utalii duniani zikiendelea kuongezeka, Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kushiriki kikamilifu katika kuvitangaza kwa manufaa ya taifa na uchumi wake.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Meneja wa Moyo Tented Camps inayomilikiwa na kampuni ya Conservation Caravan Safaris, Mary Loishooki, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa sekta binafsi katika kukuza utalii pamoja na huduma zinazotolewa na kampuni hiyo kwa wageni wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Loishooki amesema kuwa mara nyingi Watanzania wamekuwa wakivichukulia kawaida vivutio vilivyopo nchini huku wageni kutoka mataifa mbalimbali wakisafiri maelfu ya kilomita kuvitembelea, jambo ambalo linaonesha umuhimu wa wananchi kuthamini na kuvijua vivutio vyao kwa undani zaidi.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa mabalozi wa kwanza wa utalii wa Tanzania kwa kutembelea maeneo hayo, kushiriki katika kuyatangaza kupitia majukwaa mbalimbali na kuwahamasisha wengine kufanya hivyo ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na kuimarisha pato linalotokana na sekta hiyo.
“Tunapaswa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu vya utalii. Hii si kazi ya wageni pekee; sisi wenyewe tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuvitangaza kwa manufaa ya nchi yetu na vizazi vijavyo,” amesema Loishooki.
Akizungumzia huduma wanazotoa, amesema Moyo Tented Camps imeendelea kutoa huduma za malazi zenye viwango vya juu katikati ya Serengeti, ikiwawezesha wageni kufurahia mazingira ya asili kwa ukaribu zaidi huku wakipata huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Aidha, amewahimiza wadau wa utalii, kampuni za safari na wageni wanaotembelea Serengeti kutumia huduma zinazotolewa na kampuni hiyo, akisisitiza kuwa ubora wa huduma, mazingira tulivu na uzoefu wa kipekee unaopatikana katika kambi hiyo umeifanya kuwa miongoni mwa maeneo yanayovutia wageni wanaotembelea hifadhi hiyo maarufu duniani.