*Ahimiza kuwekeza kwenye miundombinu inayochochea vyanzo vya uwekezaji

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 10, 2026), wakati akizindua ghala la forodha la kampuni ya Ciwaye Trading Co. Ltd Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

“Kama tunavyoheshimu sekta ya umma, tunatakiwa kuheshimu sekta binafsi kwa uzito ule ule, kama mataifa mengine yaliyoendelea, uchumi wa mataifa hayo nguzo yake ni sekta binafsi.”

Dkt. Mwigulu aliongeza kwa kusema “Kwa kuheshimu hilo, nimeona nije kuzindua mradi huu, kama ambavyo nimepita kwenye ziara kuzindua miradi ya Serikali, ndiyo maana nimeona na hapa nije mwenyewe.”

Aidha, ameeleza kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo hauna budi kulelewa.

“Ukubwa wa jambo hili haupimwi kwa majengo, bali kwa uthubutu na matokeo yanayoakisi Dira yetu ya maendeleo na maono ya Rais wetu ya kuhakikisha mradi kama huu unatoa matokeo yaliyokusudiwa.” Amesisitiza Waziri Mkuu Mwigulu.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mradi huo unatazamwa na Serikali kama mradi wa kielelezo wa kutekeleza Dira 2050 na ndiyo maana Serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya uwekezaji nchini, ikiwemo maboresho ya sheria za uwekezaji.

“Zimebadilishwa Sheria za uwekezaji ili kuhakikisha wazawa wananufaika na kuushika uchumi, zamani vivutio vya uwekezaji viliwanufaisha wageni, lakini sasa wazawa wanapata vivutio hivyo,” ameeleza Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa: “Mfano katika sekta ya uzalishaji, zamani miradi yote mikubwa ilikuwa inatekelezwa na wageni, lakini mabadiliko hayo ya sheria yamewezesha wazawa kutekeleza miradi mikubwa, na sasa wanaweza kuajiri wageni katika utekelezaji wa miradi hiyo.”

Waziri Mkuu Mwigulu amesema mkakati mwingine unaoenda sambamba na mabadiliko ya sheria, ni pamoja na kuondoa zaidi ya tozo 270 ili kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara na walaji wa mwisho.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu ameeleza kufurahishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake, kwani umetekelezwa ndani ya muda mfupi lakini viwango vya ubora vimezingatiwa.

Amesema uamuzi wa kuanzisha ghala hilo mkoani Dodoma ni wa kimkakati kwani Dodoma ipo katikati ya nchi, ikiunganisha maeneo mengine ya nchi na fursa zilizopo katika maeneo hayo, ambapo amewataka wafanyakazi wa mradi huo kuwa waaminifu ili mradi uwe na faida endelevu, kwao binafsi na jamii.

Pia Waziri Mkuu Mwigulu amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye mikoa na maeneo yao kwa kuweka miundombinu inayochochea vyanzo vya mapato na kukua kwa uchumi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mwigulu ameuagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (TARURA) kukaa kwa haraka na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kufanya tathmini ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya kilometa 25 kuanzia Chamwino kwenda kituo cha treni cha Igandu ili kusaidia ufanisi wa ghala lililojengwa kwani barabara hiyo itaunufaisha mradi huo.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa ghala hilo, Leroy Nelson amesema mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu ambapo utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100.