Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 10 Juni 2026, Ikulu Zanzibar, amempokea mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, na kufanya naye mazungumzo Ikulu Zanzibar pamoja na ujumbe wake.

…………. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amempokea Rais wa Jamhuri ya Singapore Mhe.Tharman Shanmugaratnam,katika Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi nchini Tanzania iliyoanza Juni 8, 2026.

Kikao hicho cha ngazi ya juu kimejikita katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano wa kiuchumi kati ya Zanzibar na Singapore, hususan katika sekta zenye tija kwa maendeleo ya pande zote mbili.

Mazungumzo hayo yameangazia maeneo muhimu ya kimkakati ikiwemo utalii wa kiwango cha juu (high-value tourism), uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu, pamoja na ushirikiano katika sekta ya usafirishaji na mifumo ya ugavi (logistics), ambayo imeelezwa kuwa msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi wa kisasa.

Viongozi hao pia wamejadili namna ya kuimarisha Mpango wa Ushirikiano wa Singapore (Singapore Cooperation Programme), ambao umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa katika mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu, hususan katika sekta za maendeleo na utawala bora.

Aidha, wamekubaliana kuendeleza sekta ya usindikaji wa mazao na bidhaa ili kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo, kukuza ajira na kuimarisha ushindani wa bidhaa katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza dhamira ya Zanzibar kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia washirika wa kimataifa, akibainisha kuwa ushirikiano na Singapore ni fursa muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii pamoja na uzalishaji wa nishati hasa wa gesi asilia

Kwa upande wake, Rais wa Singapore Mhe.Tharman amepongeza juhudi za Zanzibar katika kuimarisha uchumi na ameeleza utayari wa nchi yake kuendelea kushirikiana katika sekta za utalii, teknolojia, mafunzo na uwekezaji wa kimkakati.

Ziara hiyo inaendelea kuimarisha mahusiano ya kirafiki na kiuchumi kati ya Zanzibar na Singapore, huku pande zote mbili zikieleza matumaini ya kuona ushirikiano huo ukizaa matunda zaidi kwa manufaa ya wananchi wao.