Afisa wa Udhibiti wa Ubora na Usalama wa kampuni hiyo, Julius Ngeno akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Wakati maelfu ya wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania wakikutana katika Maonesho ya Kimataifa ya Karibu-KiliFair jijini Arusha, teknolojia ya usafiri wa anga imeendelea kujitokeza kama moja ya suluhisho muhimu katika kurahisisha huduma kwa watalii na wasafiri wanaotembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii.
Miongoni mwa washiriki waliovutia macho ya wadau katika maonesho hayo ni kampuni ya usafiri wa anga ya Pro Flight Ltd Helicopters Tanzania -Kenya, ambayo imekuja na huduma za kisasa za helikopta zinazolenga kuwafikisha watu kwa haraka katika maeneo mbalimbali, hususan hifadhi za taifa, maeneo ya milimani na sehemu zenye changamoto za kufikika kwa urahisi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo, Afisa wa Udhibiti wa Ubora na Usalama wa kampuni hiyo, Julius Ngeno, amesema huduma wanazotoa zimebuniwa kwa lengo la kuongeza urahisi, usalama na ufanisi wa usafiri wa anga kwa watalii, wawekezaji na makundi mengine ya wateja wanaohitaji kufika maeneo mbalimbali kwa muda mfupi.
Amesema kampuni hiyo ilianza shughuli zake rasmi nchini Tanzania mwaka jana na imeendelea kupanua huduma zake kutokana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga, hasa kutoka kwa watalii wanaotembelea Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine vikubwa vya utalii nchini.
Ngeno amebainisha kuwa kampuni imefungua tawi jipya mkoani Kilimanjaro ili kusogeza huduma karibu zaidi na wateja, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo bila kutegemea huduma kutoka nchini Kenya kama ilivyokuwa hapo awali.
“Tumekuwa tukishuhudia ongezeko la mahitaji ya huduma za usafiri wa helikopta kutoka kwa wageni wanaokuja kutembelea Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya utalii. Kufunguliwa kwa tawi la Kilimanjaro kutasaidia kuwahudumia kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” amesema Ngeno.
Ameongeza kuwa ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho ya Karibu-KiliFair ni sehemu ya jitihada za kuonesha mchango wa teknolojia ya usafiri wa anga katika kukuza sekta ya utalii kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za haraka, salama na zenye viwango vya kimataifa.
Aidha, Ngeno amesema huduma za helikopta zimekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na matukio ya dharura yanayotokea maeneo ya milimani, hususan Mlima Kilimanjaro, ambapo baadhi ya watalii na wapandaji hukumbwa na changamoto za kiafya au ajali zinazohitaji uokozi wa haraka. Alisema uwepo wa huduma za anga husaidia kuokoa muda na kuongeza uwezekano wa kuwafikisha wahusika katika vituo vya matibabu kwa wakati.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo pia imejikita katika kutoa huduma za usafiri wa kifahari kwa watalii wanaotembelea hifadhi mbalimbali za taifa, ambapo wageni wanaweza kusafirishwa kwa helikopta hadi maeneo ya vivutio vya kipekee kwa faragha na kwa muda mfupi zaidi. Huduma hiyo imeendelea kuvutia wageni wenye ratiba maalumu pamoja na wale wanaotafuta uzoefu wa kipekee wa kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania.
Ngeno amesema kampuni imekuwa ikiandaa safari maalumu za honeymoon na matembezi ya kifahari kwa wanandoa na familia, zikiwapa fursa ya kuona mandhari ya Tanzania kutoka angani.
Amesema huduma hizo zinajumuisha safari za kutembelea wanyamapori, maeneo ya hifadhi, milima na vivutio vingine vya asili, jambo linaloongeza thamani ya uzoefu wa utalii na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa destinisheni zinazovutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.

