Mtendaji wa safari na utalii,Lucia Mbwambo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampuni hiyo jijini Arusha
………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Katika kipindi ambacho mahitaji ya huduma za safari na utalii yanaendelea kuongezeka, Kampuni ya RAISSA TRAVELS TANZANIA imeendelea kujiimarisha kwa kupanua huduma zake na kuwafikia wateja wa makundi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mtendaji wa Safari na Utalii wa kampuni hiyo, Lucia Mbwambo, amesema kampuni hiyo imeendelea kujenga rekodi nzuri ya utoaji wa huduma za kitaalamu jambo ambalo limeifanya kuaminiwa na wadau wengi wa sekta ya usafiri, utalii na biashara.
Amesema kampuni hiyo imewekeza katika utoaji wa huduma jumuishi za usafiri ikiwemo ukataji wa tiketi za ndege za ndani na kimataifa, uratibu wa safari za ndani na za Kimataifa, huduma za maombi ya viza, uwekaji wa nafasi za malazi katika hoteli mbalimbali, bima za safari pamoja na usaidizi wa pasipoti na nyaraka nyingine muhimu za usafiri.
Mbwambo amesema pamoja na huduma za kawaida za usafiri, kampuni hiyo imeendelea kujikita katika kuandaa safari maalum za makundi yenye mahitaji tofauti ikiwemo safari za ibada na hija za kidini ambazo zimekuwa zikiwavutia waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini, safari za kitalii kwa nchi mbalimbali, safari za mapumziko na fungate na nyingine nyingi kulingana na mahitaji mbalimbali.
Amebainisha kuwa mwaka huu kampuni hiyo ilifanikiwa kuratibu safari ya ibada kwa zaidi ya wanawake 50 wa Kanisa Katoliki(WAWATA) waliotembelea maeneo mbalimbali yenye umuhimu wa kiroho nje ya nchi, safari ambayo ililenga kuimarisha imani, kujifunza historia ya dini pamoja na kukuza mshikamano miongoni mwa washiriki.
Kwa mujibu wa Mbwambo, mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa kampuni katika kusimamia safari za makundi makubwa kwa ufanisi huku ikizingatia viwango vya usalama, ubora wa huduma na mahitaji ya kila msafiri, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani kwa wateja na washirika wao wa kibiashara.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi, mashirika, vikundi vya kijamii na wananchi kwa ujumla kutumia huduma zinazotolewa na RAISSA TRAVELS TANZANIA, akisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kuboresha huduma zake ili kuhakikisha wasafiri wanapata uzoefu bora, salama na wenye tija katika safari zao za ndani na nje ya nchi.
