Kiwira Mgodini, Songwe 

Bodi ya pongeza Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde Mgodi

Yaguswa na ujenzi wa madarasa

Yapongeza Uwekezaji katika mgodi wa makaa ya mawe Kiwira~ kaburo

Yahimiza Uongezaji uzalishaji wa makaa ya Mawe

Maendeleo mapya katika sekta ya madini nchini. Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sasa linatumia Akili Unde, AI, kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Kabulo Kiwira mkoani Songwe. Teknolojia hiyo imeleta mapinduzi, ikiongeza ubora wa makaa na kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi.

Ni picha tofauti kabisa sasa kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Kabulo Kiwira, uliopo Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.

Shirika la Madini la Taifa, (STAMICO) limewekeza katika teknolojia ya kisasa ya uchakataji kupitia Akili Unde, AI, pamoja na “washing plant”. Teknolojia hii ina uwezo wa kutenganisha makaa ya mawe na uchafu kwa ufanisi mkubwa. Matokeo yake: makaa safi, yenye ubora wa juu, na yanayokidhi viwango vya soko la kimataifa.

Mkurugenzi wa Migodi wa STAMICO, Mhandisi Baraka Manyama, aliwasilisha mafanikio hayo alipokuwa akiwaongoza Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, iliyofika kukagua shughuli za mgodi huo. Bodi hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Balozi, IGP Mstaafu Simon Nyakoro Sirro, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Mhandisi Manyama amesema, kabla ya utumiaji wa teknolojia hii, STAMICO ilikabiliwa na changamoto ya masoko kwa sababu ya ubora duni wa makaa. Lakini sasa, hali imebadilika.

Akaendelea Mha. Baraka Manyama: _“Baada ya kuanza kutumia teknolojia ya AI na washing plant, makaa yetu yamepata ubora. Hivi sasa tunanunuliwa na taasisi mbalimbali zinazozalisha saruji, ndani ya nchi na hata nje ya mipaka.”_

Mwenyekiti wa Bodi, Mhe. Simon Sirro, kwa niaba ya wajumbe wote, amepongeza hatua hiyo. Amesisitiza kuwa ubora wa makaa umechochea kupatikana kwa masoko mapya, na hivyo STAMICO inatakiwa kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji.

Aidha Mhe. Simon Sirro amesema:_“Tunapongeza uzalishaji wenye tija unaofanyika hapa. Teknolojia mpya imeifanya makaa kuwa na ubora. Na kwa sababu ya ubora huo, masoko yamepatikana. Tuongeze uzalishaji ili tuweze kuhudumia masoko mbalimbali.”_

Mbali na kuongeza uzalishaji, STAMICO inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii. Shirika hilo limejenga Shule ya Msingi Kapeta katika kijiji hicho. Ujenzi huo umewaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu na kusoma katika mazingira magumu, baada ya shule yao ya zamani kuchakaa na kuwa pembezoni mwa mto.

Uwekezaji wa teknolojia ya AI na kuimarisha uwajibikaji kwa jamii, ni ishara wazi kuwa STAMICO inajipanga kushindana kimataifa huku ikileta maendeleo kwa wananchi wanaozunguka migodi yake.