Na John Bukuku, Dar es Salaam

Ujio wa chapa mpya ya magari ya Jetour nchini Tanzania umetajwa kuwa hatua muhimu itakayochochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira kwa vijana na kufungua fursa mpya za biashara katika sekta ya magari na huduma zinazohusiana nayo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa magari hayo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga alisema serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kuboresha sera, sheria na mifumo ya utoaji huduma ili kuvutia uwekezaji wenye tija kwa taifa.

Alisema uwekezaji wa Jetour kupitia kampuni ya Africarriers unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda ya Taifa ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda, kwani utaongeza uzalishaji, kukuza biashara na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania.

Kapinga alisema kuingia kwa Jetour nchini hakumaanishi kuuzwa kwa magari pekee, bali ni mwanzo wa fursa mpya za uwekezaji, ajira, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya sekta binafsi nchini.

“Tunaposhuhudia uzinduzi huu, tunapaswa kutambua kuwa Africarriers na Jetour hawaleti magari pekee nchini, bali wanaleta fursa mpya za biashara, uwekezaji, ajira, maarifa ya kiteknolojia na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki,” alisema Kapinga.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo utafungua nafasi nyingi za ajira kwa vijana katika maeneo mbalimbali ikiwemo mauzo ya magari, huduma za kiufundi, huduma kwa wateja, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na sekta ya usafirishaji na magari.

Aidha, alimpongeza Africarriers Group pamoja na Jetour Global kwa kuichagua Tanzania kuwa sehemu ya safari yao ya biashara na uwekezaji, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji wote wenye nia ya kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sheria wa Kampuni za Africarriers, Ngasa Mboje alisema magari ya Jetour yameletwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la Tanzania kwa kuwa yana gharama nafuu na yanaendana na uwezo wa wananchi wengi.

Alisema kampuni hiyo imeweka mfumo wa ununuzi wa magari kwa njia ya fedha taslimu au mkopo ili kuwapa Watanzania wengi zaidi nafasi ya kumiliki magari kwa urahisi.

“Mteja anaweza kununua gari kwa mkopo na kuendelea kulitumia huku akilipa kidogo kidogo kulingana na makubaliano,” alisema Mboje.

Kapinga alisema mafanikio ya Africarriers kwa zaidi ya miaka 50 yanaonyesha uwezo na uthubutu wa wafanyabiashara wa Kitanzania, huku ushirikiano wao na Jetour ukitarajiwa kuongeza kasi ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda, biashara shindani na ajira jumuishi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.