Na Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog – Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ikibainisha kuwa hospitali hiyo imekuwa kimbilio la Wananchi na kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu maalumu nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 9, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa ziara ya kamati kukagua maendeleo ya hospitali hiyo, ikiwemo ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani, pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa.
Dkt. Lukumay amesema maboresho ya huduma chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, yameiwezesha hospitali hiyo kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini. Amesema ameona mabadiliko makubwa yanayoendelea hospitalini hapo, pia ameupongeza uongozi wa hospitali pamoja na watumishi wote kwa weledi, juhudi na kujituma katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Ameipongeza pia kwa mafanikio ya huduma ya upandikizaji uloto, ambayo tayari imenufaisha watoto 30 wenye umri wa miaka 4 hadi 12, tangu kuanzishwa Kwa huduma hio mwaka 2023.
Aidha,Amebainisha Kuwa Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha mifumo ya kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza na sugu kama saratani, figo, moyo, kisukari na magonjwa ya mifupa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema uwekezaji wa Serikali umeiwezesha BMH kutoa huduma za kibingwa 20 na ubingwa bobezi 17. Amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na programu za mafunzo kwa wataalamu kupitia Samia Scholarship.
Ameongeza kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 33 kwa ujenzi wa jengo la saratani na shilingi bilioni 4 kwa ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Awali akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, amesema hospitali hiyo imeboresha huduma na kupunguza muda wa kusubiri wagonjwa kutoka siku 2–3 hadi kati ya saa 3–6.
Amesema BMH inatoa huduma za kibingwa 20 na ubingwa bobezi 17, zikiwemo upasuaji wa moyo kwa watoto, upandikizaji figo na matibabu ya mfumo wa mkojo kwa teknolojia ya kisasa.
Aidha, amesema hospitali imeimarisha huduma kwa wateja kupitia kituo cha simu cha saa 24 na mifumo ya mawasiliano ya kidijitali, huku maabara yake ikiwa na ithibati ya kimataifa kwa mara ya tatu mfululizo.
Prof. Makubi ameongeza kuwa BMH inalenga kuwa Hospitali ya Taifa kutokana na kupanuka kwa huduma zake, huku ikiendelea na miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo kwa ufadhili wa Serikali ya Japan (shilingi bilioni 28) na mpango wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

