Na Beda Msimbe, TBN, St. Petersburg, Urusi

Tanzania inatarajia kuwasha kinu chake cha kwanza kabisa cha nishati ya nyuklia ifikapo mwaka 2029, hatua itakayoliondoa taifa katika utegemezi wa vyanzo vya kawaida vya nishati na kuingia katika ukurasa mpya wa nishati ya uhakika kwa ajili ya mapinduzi ya viwanda na uchumi.

Hayo yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na waandishi wa habari walioambatana naye katika ziara ya kikazi nchini Urusi.

Rais Samia alisisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuona kuwa kabla ya mwaka 2029, kinu hicho kiwe kimeanza rasmi shughuli zake, huku nchi ikidhamiria kutumia nishati hiyo inayotokana na madini ya urani yaliyopo nchini.

Akijibu swali kuhusu hitaji la kwanza katika teknolojia ya nyuklia, Rais Samia alisema taifa linahitaji uzoefu wa Urusi katika nyanja zote zinazohusu teknolojia hiyo, ikiwemo maandalizi ya taifa kutumia umeme unaozalishwa kutokana na urani.

Nishati ya nyuklia inatazamwa kama nguzo kuu ya “nishati ya uhakika kwa maendeleo” (reliable energy for development). Tofauti na vyanzo vya maji vinavyotegemea mabadiliko ya tabianchi au mafuta yanayoyumba bei katika soko la dunia, nyuklia huzalisha umeme thabiti (baseload power) unaopatikana muda wote kwa ajili ya kuendesha viwanda vizito, mifumo ya usafirishaji kama reli ya kisasa ya SGR, pamoja na miji ya kisasa. Huu ndio msingi wa nishati endelevu inayochochea maendeleo ya haraka bila kukwama.

Katika mazungumzo yaliyofanyika tayari, Kampuni ya Tanesco imeingia makubaliano ya kutunza siri za mazungumzo na kampuni ya Kirusi ya Rosatom, ambayo imeeleza utayari wake wa kuiwezesha Tanzania kupata umeme wa kutosha na wa uhakika.

Katika kufanikisha azma hiyo ya kuwa na nishati ya nyuklia kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa kuhusu matumizi ya amani ya teknolojia hiyo, Rais Samia alieleza kuwa kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kujenga uwezo wa ndani (local capacity) kupitia elimu.

Alibainisha kuwa tayari kuna kundi la Watanzania wanaosomea uhandisi wa nyuklia nchini Urusi chini ya udhamini wa kampuni ya Mantra Tanzania, lengo likiwa ni kuwa na wataalamu wazawa watakaofahamu mifumo yote na kuweza kuendesha mitambo hiyo hata baada ya wataalamu wa kigeni kuondoka.

Mbali na nishati, makubaliano hayo mapya yanakusudia pia kufufua miradi ya kiteknolojia iliyokuwa imesimama. Rais aligusia azma ya kufufua ushirikiano wa kinyuklia katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), mradi ambao hapo awali ulisuasua kutokana na changamoto za washirika wa mwanzo, lakini sasa Urusi ipo tayari kuingia kati na kuusukuma mbele kwa matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia.