Farida Mangube, Morogoro
Wataalamu wameonya kuwa kuongezeka kwa matumizi ya kemikali za kilimo bila kuzingatia kanuni za kitaalamu kunaweza kuongeza hatari ya magonjwa, kuathiri ubora wa mazao na kuhatarisha mazingira, wakitaka wakulima kuelekea zaidi katika matumizi ya mbinu za kilimo ikolojia.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Sekretarieti ya Kitovu cha Kilimo Ikolojia kupitia Mradi wa Mtandao wa Utafiti wa Ikolojia Kusini mwa Afrika (RAENS) mkoani Morogoro, Profesa Kalunde Sibuga wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) alisema matumizi yasiyo sahihi ya kemikali yanaweza kuathiri afya za wakulima, walaji na mazingira, huku mabaki ya kemikali kwenye mazao yakihatarisha usalama wa chakula.
Alisema kilimo ikolojia ni suluhisho linaloweza kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira kama mbolea za asili, udhibiti wa wadudu kwa njia za kibaiolojia na usimamizi endelevu wa ardhi na maji, akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi salama ya pembejeo.
Kwa upande wake, Mratibu wa RAENS, Profesa Dismas Mwaseba, alisema pamoja na uwepo wa sera zinazounga mkono kilimo endelevu, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto zikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika, uelewa mdogo wa wakulima na upungufu wa huduma za mafunzo na ugani kuhusu kilimo ikolojia.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gosbert Chobya, alisema Serikali inaendelea kutambua mchango wa kilimo ikolojia katika kuongeza tija, kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku akisisitiza ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuboresha sera na mazingira ya utekelezaji wa kilimo hicho nchini.

