OWM-TAMISEMI, Iringa
Serikali imeendelea kuelekeza nguvu katika kuibua na kukuza vipaji vya michezo nchini kwa lengo la kuandaa kizazi cha wanamichezo kitakachoiwakilisha na kuiletea heshima Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza katika Baraza la Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania (UMITASHUMTA) lililofanyika Juni 7, 2026 mkoani Iringa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndg. Amos John, alisema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya michezo na tayari matokeo ya uwekezaji huo yameanza kuonekana.
“Matokeo ya uwekezaji huu yanaonekana wazi kupitia timu ya Serengeti Boys chini ya miaka 17 iliyoshiriki Fainali za AFCON 2026 nchini Morocco. Tunatarajia kutumia mashindano haya ya mwaka huu kupata wachezaji wengi zaidi watakaotumika katika timu mbalimbali za Taifa siku zijazo,” alisema Amos.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Michezo, Utamaduni na Sanaa wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Ndg. Yusuph Singo, alisema maandalizi ya mashindano ya UMITASHUMTA 2026 yamekamilika kwa mafanikio.
Alibainisha kuwa washiriki wote kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar wamewasili na kupokelewa tayari kwa kuanza mashindano hayo.
“Lengo la Baraza la UMITASHUMTA ni kukumbushana masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa wakati wote wa mashindano haya ili kuhakikisha yanafanyika kwa utulivu, usalama na mafanikio makubwa,” alisema Singo.
Mashindano hayo yanayowakutanisha wanamichezo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Unguja na Pemba, yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Juni 9, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe.
UMITASHUMTA na UMISSETA 2026 yanaandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, yakiwa na kaulimbiu isemayo:
“Michezo na Sanaa Shuleni: Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa.”

