Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro Mkoani Manyara, akiwa kwenye mkutano wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, kulia kwake ni mfanyabiashara wa Mji mdogo wa Mirerani, Agnes Lema (Mama Swai hardware).
…………
Na Mwandishi wetu, Mirerani
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro Mkoani Manyara, amekemea vikali uuzwaji holela wa ardhi unafanywa baadhi ya viongozi wa vijiji.
Ole Millya ameyasema hayo katika Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro, kwenye ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Laban Kihongosi alipohitimisha ziara yake ya siku tatu Mkoani Manyara.
Amesema tatizo la uuzwaji holela wa ardhi katika wilaya ya Simanjiro, limekuwa kero kwani baadhi ya viongozi wa vijiji wenye tamaa wanagawa ardhi kwa maslahi yao
“Baadhi ya wenyeviti wanauza ardhi bila kushirikisha mkutano mkuu wa kijiji na baadhi ya wenyeviti wastaafu wanatembea na mihuri na mihutasari iliyopita katika uuzaji wa ardhi,” amesema Ole Millya.
Ameeleza kwamba wakati mwingine anaona ni vyema hata miradi ya maendeleo isifanyike kwa muda wa mwaka mmoja ili viongozi na jamii kwa ujumla ishuhulikie migogoro ya ardhi.
“Tuna Mkuu wa Mkoa wa Manyara mzuri sana Queen Cuthbert Sendiga lakini peke yake hataweza, tuna Mkuu wa Wilaya bora kabisa Fakii Raphael Lulandala ila mwenyewe hataweza hivyo chama na Serikali tukae pamoja kuangalia hilo,” amesema Ole Millya.
Hata hivyo, Kenani akizungumza na baadhi ya wakazi wa eneo hilo amesema chama hicho kinaelekeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga kuhakikisha anavalia njuga changamoto hiyo.
“Chama kinaelekeza kuwa Mhe Mkuu wa Mkoa wa Manyara, atafuatilia na kusikiliza migogoro ya ardhi iliyopo kisha atatupatia mrejesho na DC Simanjiro Mhe Lulandala ataanza kesho kwenye kata hii,” amesema Kenani.
