mzalishaji wa miche ya kisasa ya kahawa aina ya Arabika kompacti wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Mussa Mdaka kulia na mkulima wa kahawa Frank Hyera,wakiondoa uchafu kwenye kitalu cha miche ya kahawa ili kuruhusu miche kustawi vizuri.

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

BAADHI ya wakulima wa zao la kahawa katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wameishukuru serikali kupitia bodi ya kahawa Tanzania(TCB)kwa kuwapa miche ya kisasa ya kahawa aina ya Arabika compact yenye tija kubwa ikilinganisha na miche ya kienyeji.

 

Wakulima hao wamesema,miche hiyo inayotolewa bure na serikali imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi kutokana na uzalishaji wake kuwa mkubwa, hivyo kupunguza umaskini kwenye familia nyingi zinazotegemea zao la kahawa kuendesha maisha yao.

 

Desderia Ndunguru alisema,miche hiyo ina uwezo wa kuzalishaji kilo 15 hadi 20 kwa mti mmoja, jambo linalohamasisha wananchi wengi hususani vijana kujikita kwenye kilimo cha zao la kahawa wilayani Mbinga.

 

“Miche hii tunapata dumla 4 hadi tano sawa na kilo 15 kwa mti mmoja tofauti na ile ya kienyeji,tunaishukuru sana serikali yetu kutuletea miche ya kisasa ambayo tunagawiwa bure,gharama ambayo ingetumika kununua miche tunatumia kununua mashamba na kwenye gharama nyingine ikiwemo mbolea na dawa za kuuwa wadudu”alisema Ndunguru.

 

Mkulima mwingine Frank Hyera alisema,ugawaji wa miche hiyo bora utaleta chachu ya kilimo cha zao la kahawa na kuongeza uzalishaji katika wilaya ya Mbinga hivyo kuwakwamua wananchi wengi kiuchumi.

 

Hyera,ameiomba serikali kupitia wizara mama ya kilimo iendelee na mpango wa kuzalisha na kugawa miche hiyo bure ili kuhamasisha watu wengi zaidi waendelee kupanda ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

 

Alisema,miche aina ya arabica compact inazaa kwa muda mfupi wa miaka miwili hadi mitatu ikilinganishwa na miche ya zamani ambayo inachukua muda mrefu na uzalishaji wake ni mdogo.

 

Mmoja wa wazalishaji wa miche hiyo Mussa Mdaka alisema,ameamua kuzalisha miche hiyo baada ya kupata sapoti kutoka kwa bodi ya kahawa Tanzania na anaigawa bure kwa wakulima wanaokwenda kupanda kwenye mashamba yao.

 

Mdaka alisema,amehamasika kuzalisha miche hiyo hasa baada ya wakulima wengi kuhitaji kutokana na zao la kahawa kuwa na bei nzuri kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

 

“Kitalu hiki nazalisha miche milioni moja na inagawanywa kwa wakulima wa Mbinga mjini na vijijini,lengo likiwa kuwapunguzia gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa zao hili katika wilaya yetu ya Mbinga”alisema Mdaka.

 

“Miche hii ni ya muda mfupi,wakulima wakipanda baada ya miaka miwili wataanza kuvuna kahawa,lakini ili waweze kufikia lengo lazima waitunze vizuri na watambue namna unavyoitunza ndiyo unavyozalisha kahawa nyingi”alisema Mdaka.

 

Amewataka wakulima kuhakikisha wanazingatia kanuni za kilimo na utunzaji wa kahawa ili waweze kuzalisha kwa tija na kupata bei nzuri na kuwaomba maafisa ugani wawatembelea wakulima na kuwapa ushauri wa kitaalamu ili waondokane na kilimo cha mazoea na walime kwa tija.

“Tunahitaji wataalamu wawafikiea wakulima wawape elimu ili waweze kulima kilimo chenye tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa,kwani kahawa ni dhahabu,inalipa sana pale mkulima anapopewa elimu na kufuata kanuni na taratibu za kilimo cha zao hili”alisema.

Kwa mujibu wa takwimu za bodi ya kahawa Tanzania(TCB)uzalishaji wa kahawa katika wilaya ya Mbinga kwa sasa ni tani 25,000 kwa mwaka na ugawaji wa miche hiyo utaongeza uzalishaji hadi kufikia zaidi ya tani 28,000 katika wilaya hiyo huku malengo kitaifa ya uzalishaji hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka 2025/2026.Muonekano wa kitalu cha miche mipya ya kahawa aina ya Arabika kompact inayozalishwa na Mussa Mdaka na kugawiwa kwa wakulima bure