.Na ABDU MADENGE, WAF – DODOMA
Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini limefuta usajili wa dawa ya Powaful Banana Medicine, kupiga marufuku uingizwaji na matumizi ya dawa ya Vitamax, pamoja na kuamuru kuondolewa sokoni kwa toleo namba MN1060 la dawa ya Joy.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya ukaguzi na vipimo vya maabara kubaini uwepo wa mchanganyiko wa kemikali hatari za kisasa na sumu kuvu kwenye bidhaa hizo kinyume cha sheria.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Nicolao Joseph Otieno, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya Juni 05, 2026 Mkoani Dodoma ambapo ameeleza maamuzi hayo yanajiri kufuatia zoezi maalum la ufuatiliaji wa dawa sokoni (Post Market Surveillance) lililofanyika katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, ambalo lilibaini ukiukwaji mkubwa wa Kanuni za Usimamizi wa Dawa za Tiba Asili kifungu cha 13(1)(a) na (b).
Prof. Otieno ameongeza kuwa Uchunguzi wa kimaabara umeonesha dawa ya Powaful Banana (inayotengenezwa na Powaful Products Company Ltd) na Vitamax (kutoka kampuni ya Superfood International ya Malaysia), ambazo zimekuwa zikitumika kuongeza nguvu za kiume, zimechakachuliwa kwa kuongezewa kemikali za kisasa za Sildenafil, Tadalafil, pamoja na dawa za maumivu aina ya Tramadol na Paracetamol.
“Tunaonya matumizi ya kemikali hizo bila usimamizi wa daktari yanaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kufeli kwa ini na figo, shinikizo la damu, na hata vifo vya ghafla.” amesema Prof . Otieno.
Sambamba na hatua hizo, Baraza pia limebaini kuwa toleo namba MN1060 la dawa ya Joy (Usajili Na. TZ25TM0010) lina kiwango kikubwa cha sumu kuvu (mycotoxins) kinachoweza kusababisha saratani ya ini na uharibifu wa figo. Hali hii imetajwa kutokana na kutokuzingatiwa kwa viwango bora vya ukaushaji na uhifadhi wakati wa uzalishaji.
“Baraza tunatoa onyo kali kwa watengenezaji wote nchini ambao dawa zao zimebainika kuwa na mapungufu katika vifungashio, taarifa za lebo, ujazo, na maelezo ya dozi, tunawataka kufanya maboresho ya haraka kulingana na vigezo vya usajili kwa lengo la kulinda afya na usalama wa watumiaji.” amesema na kuongeza Prof. Otieno.


