Farida Mangube, Morogoro

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imebaini dosari katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato na kufanikisha kurejeshwa kwa zaidi ya Shilingi milioni 69 ambazo zilikuwa hazijakusanywa, hatua inayodhihirisha juhudi za taasisi hiyo katika kulinda mapato ya serikali na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga, alisema kiasi cha Shilingi 69,248,392 kilikusanywa baada ya operesheni maalumu ya kufuatilia makusanyo ya mapato kupitia mashine za POS zinazotumia mfumo wa TAUSI. 

Alisema uchunguzi ulibaini kutokuwiana kwa taarifa za makusanyo kati ya mfumo huo na taasisi za kifedha, hali iliyosababisha kuonekana kwa madeni yasiyo halisi kabla ya dosari hizo kurekebishwa.

 Taasisi hiyo pia ilifuatilia utekelezaji wa miradi minane ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.7 kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana. 

Aliongeza kuwa ushauri wa kitaalamu uliotolewa na TAKUKURU uliwezesha kuokolewa au kurejeshwa matumizi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 15.7 katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.

Kwa upande wa elimu kwa umma, alisema TAKUKURU iliendesha semina 74, mikutano ya hadhara 19 na kuhamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa klabu 100 za kupinga rushwa. Aidha, taasisi hiyo ilipokea malalamiko 94 kutoka kwa wananchi, ambapo 65 yalihusu tuhuma za rushwa na kuanza kufanyiwa kazi, huku 29 yakielekezwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya bure 113, simu 0738 150 143 au katika ofisi za taasisi hiyo zilizo karibu nao. Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wamepongeza juhudi hizo wakisema zimechangia kuokoa fedha za umma na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.