Dkt. Immaculate Aware Semesi Mkurugaaenzi Mkuu Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) (kushoto) akiwa na Novatus Mushi Meneja wa Kanda ya Kati NEMC katika banda la taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliyofanyika Jakaya Kikwete Convetion Center jijini Dodoma Juni 05, 2026.
…………
Na John Bukuku, Dodoma
Bw Novatus Mushi, Meneja wa Kanda ya Kati wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), amesema zaidi ya wananchi na wadau mbalimbali 400 wametembelea banda la NEMC na kupata elimu ya utunzaji wa mazingira wakati wa Wiki ya Mazingira Duniani. Hatua hiyo imelenga kuongeza uelewa wa jamii katika kuijenga Tanzania ya kijani na kuimarisha usimamizi wa mazingira ya kidijitali.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Juni 05, 2026, Mushi amesema mwamko huo wa wananchi na wadau mbalimbali unaonesha ongezeko la uelewa kuhusu umuhimu wa elimu ya mazingira na mchango wake katika kubadili mitazamo ya jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira nchini.
Amesema NEMC imeendelea kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali inayowezesha ufuatiliaji wa masuala ya mazingira kwa wakati halisi (real time), ikiwemo mfumo unaoonesha dalili au viashiria vya uchafuzi wa mazingira pindi vinapotokea.
“Tunazo mifumo ya kisasa ya usimamizi wa mazingira ya kidijitali. Kwa mfano, kuna mfumo mpya kabisa tunaouonyesha hapa, unaotuwezesha kuona dalili au viashiria vya uchafuzi wa mazingira kwa wakati halisi (real time). Mfumo huu unasaidia sana katika ufuatiliaji wa mazingira,” amenukuliwa akisema Mushi.
Amefafanua kuwa pamoja na mfumo huo, NEMC pia inatumia mfumo wa utoaji wa vibali vya miradi, hususan vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), kabla ya kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, ili kuhakikisha mazingira yanalindwa tangu hatua za awali za utekelezaji.
“Tunatumia pia mfumo wa PMS unaosaidia katika utoaji wa vibali, hususan vibali vya tathmini ya mazingira kabla ya mradi kuanza. Hii inarahisisha sana kazi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazingira,” ameongeza.
Mushi amesema maonyesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wadau mbalimbali waliotembelea banda la NEMC, ambapo zaidi ya watu 400 wamepata fursa ya kujifunza namna teknolojia inavyoweza kuboresha usimamizi wa mazingira.
Aidha, ameeleza kuwa NEMC inashirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuimarisha ubadilishanaji wa takwimu za hali ya hewa na mazingira, hatua inayosaidia kufanya maamuzi sahihi ya maendeleo na kuokoa gharama zinazoweza kupotea kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi.
“Tumekuwa na programu shirikishi na TMA ambazo zinatusaidia kupata takwimu sahihi za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa. Hii inasaidia sana kuokoa mabilioni ya fedha ambazo zingepotea endapo miradi ingetekelezwa bila kuzingatia takwimu hizo,” amesema.
Akizungumzia hatua ya taasisi hiyo kuelekea kuwa mamlaka kamili, Mushi amesema itasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kupunguza urasimu na kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.
“Pale tutakapokuwa mamlaka, tutatekeleza malengo ya dira kwa ufanisi zaidi. Mazingira, watu na uchumi lazima viendane. Tukipata mamlaka, tutapunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,” amesema.
Kuhusu hali ya mazingira katika Kanda ya Kati, Mushi amesema kanda hiyo inayohudumia mikoa ya Dodoma, Iringa na Singida, yenye takribani watu milioni saba, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya vifaa duni katika shughuli za kiuchumi, migogoro ya matumizi ya ardhi na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Amesema NEMC itaendelea kuimarisha ufuatiliaji, elimu kwa umma na usimamizi wa sheria ili kuhakikisha rasilimali za mazingira zinalindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


