Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kufanya doria za kubaini na kuzuia uhalifu. Pia oparesheni na misako imeendelea kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.
Kwa kipindi cha mwezi Mei, 2026 jumla ya watuhumiwa 871 wa uhalifu ikiwemo Mauaji, kujeruhi, kubaka, kupatikana na silaha bila kibali, kupatikana na dawa za kulevya na matukio ya wizi walikamatwa. Watuhumiwa waliokamatwa na upelelezi wa kesi zao kukamilishwa walifikishwa Mahakamani na baadhi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili, Baraka Mwakatobe [31] na Said Baraka [39] wote wakazi wa Dodoma kwa tuhuma za kupatikana na vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini.
Watuhumiwa walikamatwa Mei 28, 2026 saa 8:30 usiku katika kizuizi cha Polisi cha Chimala, Wilaya ya Mbarali katika Barabara kuu ya Mbeya – Njombe wakiwa na shehena ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini boksi 403 vya aina mbalimbali wakivisafirisha kwa Gari yenye namba za usajili T.997 ERG aina ya Canter kutoka Tunduma Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe kuelekea Mkoa wa Dodoma.
Watuhumiwa walikutwa na vitenge vikoi jozi 03 vilivyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru wa forodha kutoka nchi jirani. Upelelezi unakamilishwa ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Shaban Safari [48] mkazi wa Mtaa wa Roma Kyela Kati kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroine kete 27.
Mtuhumiwa alikamatwa Juni 2, 2026 saa 3:30 usiku maeneo ya Mtaa wa Roma, Kata ya Kyela Kati, Tarafa ya Unyakyusa, Mkoa wa Mbeya akiwa na dawa hizo za kulevya aina ya Heroine na Bhangi yenye uzito wa Gramu 2 akiwa ameweka kwenye mfuko wa khaki. Mtuhumiwa ni muuzaji wa dawa hizo za kulevya.
Sambamba na hayo, kwa kipindi cha mwezi Mei, 2026 jumla ya watuhumiwa 20 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kilo 12.24, watuhumiwa 2 walikamatwa wakiwa na pombe haramu ya moshi maarufu Gongo lita 30, watuhumiwa 2 walikamatwa wakiwa na Silaha aina ya Gobole likiwa na Goroli 7, watuhumiwa ni wawindaji haramu katika hifadhi za taifa.
Kwa kipindi cha mwezi Mei, 2026 jumla ya kesi zote zilizofikishwa mahakamani zilikuwa 224, kesi 122 zilipata mafanikio kwa washitakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo. Aidha, kesi 73 bado zipo mahakamani katika hatua mbalimbali.
Katika Mahakama ya Kuu Kanda ya Mbeya, Barnaba Daud Mtweve [56] mkazi wa Chunya amepatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa matatu ya kuua watu wawili aliyoyatenda dhidi ya aliyekuwa mzazi mwenzake aitwaye Herriety Lupembe [37] aliyekuwa Mwalimu katika Shule ya Msingi Mbugani, Ivone Tatizo [15] aliyekuwa Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Isenyela na kujaribu kumuua Mtoto wake aitwaye Harris Barnaba Mtweve [06] Mwanafunzi wa Darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Ken Gold.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe Joachim Charles Tiganga Juni 3, 2026. Kabla ya hukumu hiyo ilielezwa kuwa Mshitakiwa alitenda makosa hayo Machi 31, 2024 ssa 2:30 usiku huko Kijiji cha Kiwanja, Kata ya Mbugani, Wilayani Chunya baada ya kuingia ndani ya nyumba aliyekuwa akiishi mzazi mwenzake Herriety Lupembe, Mtoto Ivone Tatizo na Mtoto Harris Barnaba kisha kuwapiga kwa kitu butu kichwani na kusababisha kupoteza maisha huku mtoto Harris Barnaba [06] akimjeruhi na kisha kufunga milango kwa nje kuondoka na funguo za milango.
Waendesha Mashitaka wa Serikali Wakili Rajabu Msemwa, Wakili George Seni na Wakili Dominick Mushi wakiwa mahakamani hapo waliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe funzo kwa watu wengine wenye tabia kama hizo ili kukomesha vitendo vya mauaji na ukatili kwa watoto katika jamii.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na mikakati ya kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani kwa kuhakikisha Madereva na watumiaji wengine wa barabara wanapata elimu ya usalama barabarani, Madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani wanakamatwa na kuchukulia hatua kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani.
Aidha, kwa kipindi cha mwezi Mei, 2026 jumla ya madereva 09 wamefungiwa leseni za udereva kutokana na kusababisha ajali na kutenda makosa hatarishi ikiwemo mwendo kasi na kuyapita magari mengine katika maeneo hatarishi (Wrong Overtaking) na kuhatarisha usalama wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia na kutokomeza uhalifu. Aidha, linatoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi ili washitakiwa waweze kutendewa kwa mujibu wa sheria. Pia linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi wanaoendelea kujihusisha na uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi.

