Ofisi ya Taifa ya Takwimu – NBS kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania – TASAC, zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano – MoU kufanya Sensa ya Vyombo vya Usafiri wa Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara Mwaka 2026/2027 ili kupata Takwimu rasmi zitakazosaidia kuboresha usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano huo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ngorongoro uliopo Jengo la Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma tarehe 03 Juni 2026, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa amesema hiyo ni hatua muhimu itakayowezesha uratibu wa mfumo wa Takwimu rasmi nchini na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya kuiwezesha Serikali na wadau kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa Wananchi.
Dkt. Amina Msengwa, amesema sensa hiyo itasaidia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali, ikiwemo kuimarisha mfumo wa usafirishaji fungamanishi nchini ambapo Takwimu zinazopatikana kupitia sensa hiyo zitakuwa ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kupanga uwekezaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, amesema sensa hiyo ni hatua muhimu katika kuhuisha kanzidata ya kitaifa ya vyombo vya usafiri majini na kupata taarifa sahihi kuhusu vyombo vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
Takwimu zitakazopatikana zitatumika kuimarisha usalama wa vyombo na abiria, kuboresha upangaji wa miundombinu ya usafiri majini, kuchochea uwekezaji katika uchumi wa buluu na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Sensa hiyo itakuwa ya pili kufanyika nchini baada ya sensa ya kwanza iliyofanyika Mwaka 2021 kwa ushirikiano wa NBS na TASAC.

