Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bi. Jana Bricco, baada ya kufika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaaam, kujitambulisha akiambatana na Mwakilishi Mkazi aliyemaliza muda wake Bw. Sebastian Acevedo (hayupo pichani).

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Katikati), Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bi. Jana Bricco, na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo aliyemaliza muda wake Bw. Sebastian Acevedo, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaaam, ambapo Mwakilishi huyo mpya alifika kwa ajili ya kujitambulisha.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Katikati), Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bi. Jana Bricco (wa pili Kushoto), Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo aliyemaliza muda wake Bw. Sebastian Acevedo (wa pili kulia), Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade (Kushoto) na Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Fedha za Nje, Bi. Mukajungu Kamuzora (Kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaaam, ambapo Mwakilishi huyo mpya alifika kwa ajili ya kujitambulisha (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

………….

Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bi. Jana Bricco, katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaaam, aliyefika kujitambulisha akiambatana na Mwakilishi Mkazi aliyemaliza muda wake Bw. Sebastian Acevedo. Bi. Jana Bricco, anayetarajiwa kuanza kazi mwezi Agosti 2026 aliteuliwa mwezi Machi 2026 kuliwakilisha Shirika hilo nchini Tanzania.

Katika mazungumzo yao walijadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano imara uliopo kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya Fedha duniani, katika ufadhili na kutekeleza miradi ya kimkakati pamoja na programu mbalimbali, kusimamia na kuimarisha uchumi.

Aidha walitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mwakilishi Mkazi aliyemaliza muda wake, Bw. Sebastian Acevedo kwa kazi yake nzuri ya kuiwakilisha Taasisi hiyo na kuendelea kujenga uhusiano thabiti kati ya IMF na Tanzania.

Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2026, uwekezaji wa mikopo na misaada wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwa Tanzania umefikia SDR bilioni 3.27 sawa na dola za Marekani takribani bilioni 4.64, zilizoelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia Bajeti Kuu ya Serikali.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade na Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Fedha za Nje, Bi. Mukajungu Kamuzora.