WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Muhandisi Hamad Yusuf Masauni akizungumza na vijana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya siku ya maziniea na fursa zinazopatikana katika mnyororo mzima wa mazingira. 
Dkt. Immaculate Sware Semesi. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wa tatu kutoka (kulia) ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika kongamano hilo la vijana lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
………….
Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Muhandisi Hamad Yusuf Masauni, amewataka vijana nchini kutumia ubunifu, teknolojia na maarifa yao kunufaika na fursa zinazotokana na sekta ya mazingira badala ya kusubiri ajira za Serikali pekee.
Akifungua Kongamano la Vijana kuhusu Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira lililofanyika leo Juni 2,2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Masauni amesema mazingira si suala la uhifadhi pekee bali ni chanzo kikubwa cha ajira, biashara na maendeleo ya kiuchumi kwa vijana.
Amesema vijana wanapaswa kuelewa kuwa changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kubadilishwa kuwa fursa za kujipatia kipato kupitia biashara ya kaboni, urejelezaji wa taka, matumizi ya nishati safi, utunzaji wa mikoko, kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi na teknolojia za kijani.
Masauni amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira huku ikikuza uchumi wa kijani unaolenga kuongeza ajira na ustawi wa wananchi.
Amebainisha kuwa vijana ndio watakaobeba athari kubwa za uharibifu wa mazingira siku zijazo, hivyo wana wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunataka kila kijana aelewe kuwa mazingira ni utajiri. Ukiona taka, usione uchafu pekee, ona fursa ya biashara. Ukiona mikoko, usione miti tu, ona rasilimali inayoweza kuchangia mapato kupitia biashara ya kaboni,” amesema Masauni.
Aidha, amewataka vijana kutumia mitandao ya kijamii na teknolojia za kisasa kutafuta masoko, kuandaa miradi ya mazingira na kuvutia uwekezaji badala ya kutumia muda mwingi katika shughuli zisizo na tija.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, amesema vijana ni nguvu kubwa ya mabadiliko katika bara la Afrika kutokana na idadi yao kubwa, hivyo ushiriki wao katika masuala ya mazingira ni muhimu kwa maendeleo endelevu.
Amesema Serikali imefanikiwa kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kituo cha Vijana wa Afrika cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi, hatua itakayowajengea vijana uwezo katika utafiti, ubunifu, diplomasia ya mazingira na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira, Kemirembe Mutasa, amesema Serikali imeweka sera, sheria na miongozo mbalimbali inayolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kongamano hilo lililowakutanisha wanafunzi wa Sekondari na vyuo vikuu, taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, limefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yenye kaulimbiu ya Tanzania ya mwaka 2026 isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kupigania Tanzania.”

