Bohari ya Dawa (MSD) inatarajia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa mwaka, ambazo kwa sasa hutumika kugharamia ukodishaji wa maghala binafsi kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa za afya.
Tathmini hiyo imetolewa na uongozi wa MSD baada ya kukabidhi rasmi hati ya mradi wa ujenzi wa ghala jipya la kisasa pamoja na kibali cha ujenzi kwa Kampuni ya Hainan International kutoka China, itakayotekeleza mradi wa ujenzi wa ghala hilo la kisasa kwa Kanda ya Dar es Salaam.
Ghala hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 3,900 linajengwa katika eneo la Keko, karibu na Makao Makuu ya MSD mkoani Dar es Salaam, na linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, alisema ujenzi wa ghala hilo umezingatia matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na nishati mbadala kwa lengo la kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, kupunguza gharama za uendeshaji na kuunga mkono jitihada za uhifadhi wa mazingira.
Aliongeza kuwa fedha zote za utekelezaji wa mradi huo tayari zimetengwa, jambo linalotoa uhakika wa mradi kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Aidha, alisema kukamilika kwa ghala hilo kutaimarisha uwezo wa MSD katika kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya, kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja na wadau wa sekta ya afya, pamoja na kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wananchi.

