Watumiaji wa petroli wamepata afueni mwezi Juni 2026 baada ya bei ya mafuta hayo kushuka ikilinganishwa na mwezi uliopita. Kwa Dar es Salaam, petroli sasa itauzwa kwa bei kikomo ya shilingi 4,086 kwa lita, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama kwa watumiaji wa kawaida na baadhi ya shughuli za usafiri.

Kwa upande wa dizeli, watumiaji wanakabiliwa na ongezeko dogo la bei, ambapo kwa Dar es Salaam bei kikomo imefikia Shilingi 4,333 kwa lita. Ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia pamoja na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa hiyo.

Licha ya changamoto hizo za kimataifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kulinda uchumi na wananchi kwa kuweka ruzuku ya Shilingi 534.91 kwa kila lita ya dizeli. Hatua hiyo imelenga kupunguza athari za ongezeko la bei kwa sekta muhimu kama usafirishaji, viwanda na huduma za kijamii.

Mabadiliko haya yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, vinavyohusisha Marekani, Israeli na Irani. Mgogoro huo umeathiri uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa mafuta duniani, huku kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kukiongeza gharama za usafirishaji na bima za meli za mafuta.