Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaosimamia masuala ya mtangamano wamekutana katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) ngazi ya mawaziri, unaotarajiwa kufanyika tarehe 4 Juni 2026.
Kikao hicho cha Makatibu Wakuu, kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 2 hadi 3 Juni 2026, ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya mkutano wa mawaziri unaotarajiwa kutoa mwelekeo wa kisera na maamuzi yatakayochochea ukuaji wa biashara, maendeleo ya viwanda na ongezeko la uwekezaji katika Jumuiya, sambamba na kuimarisha ushindani wa uchumi wa kanda.
Makatibu Wakuu hao wamepokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa SCTIFI. Miongoni mwa taarifa zilizojadiliwa ni pamoja na; taarifa Kamati ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Ushindani ya Afrika Mashariki na Kamati ya Maendeleo ya Viwanda.
Aidha, kikao hicho kimejadili taarifa ya mapitio ya Kanuni za Uasili wa Bidhaa za Afrika Mashariki (Rules of Origin) iliyowasilishwa na Kikosi Kazi cha Kikanda cha Wataalamu. Mapitio hayo pamoja na masuala mengine yanalenga kulinda soko la bidhaa zinazozalishwa ndani ya EAC kwa kuhakikisha bidhaa zinazostahili kunufaika na upendeleo wa biashara ndani ya Jumuiya. Hatua hiyo pia inalenga kuchochea uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, kuvutia uwekezaji wa viwandani na kuimarisha ushindani wa bidhaa za EAC katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Baraza hili ni moja ya vyombo muhimu vya maamuzi katika Jumuiya chenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa ajenda za mtangamano wa kiuchumi. Baraza hilo husimamia maendeleo ya Soko la Pamoja, Umoja wa Forodha na mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza biashara ya ndani ya Jumuiya, kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kodi (NTB’s), kuimarisha ushindani wa viwanda vya kikanda na kuvutia uwekezaji unaochochea ukuaji wa uchumi na ajira.
SCTIFI imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha biashara ya kikanda kwa kuwezesha urahisishaji wa biashara mipakani, kurasinisha viwango vya bidhaa, kuimarisha mifumo ya forodha na kuendeleza sera zinazolenga kukuza sekta binafsi na ushiriki wa wawekezaji katika maendeleo ya uchumi wa Jumuiya.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, ukijumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides R. Mbwasi, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.

