Na. Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali ya kodi yanayolenga kuongeza mapato ya ndani, kupanua wigo wa walipakodi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Juni 2, 2026, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar amesema kuwa mageuzi hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga mfumo wa kodi wenye ufanisi zaidi na unaochochea ukuaji wa uchumi.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera, sheria na taratibu za kodi ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unakuwa endelevu huku ukipunguza usumbufu kwa walipakodi na wawekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi yameendelea kuimarishwa kwa lengo la kuongeza uwazi, kudhibiti ukwepaji kodi na kupunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Pia ameongeza kuwa mageuzi hayo yanakusudia kujenga mazingira rafiki ya biashara yatakayowezesha sekta binafsi kukua, kuvutia uwekezaji zaidi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Amesema Kuwa Serikali itaendelea kusimamia mageuzi hayo ili kuhakikisha mfumo wa kodi unakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi badala ya kuwa kikwazo kwa uzalishaji na uwekezaji.
Ameeleza kuwa mafanikio ya mageuzi hayo yataongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
