Na. Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

 Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa fedha za umma na ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika taasisi za Serikali.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kuwa matumizi ya teknolojia yamekuwa sehemu muhimu ya mageuzi yanayoendelea kufanyika katika sekta ya fedha nchini.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha na kuunganisha mifumo mbalimbali ya kidijitali ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma.

Aidha, amebainisha kuwa mifumo hiyo imechangia kudhibiti upotevu wa mapato, kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Serikali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa walipakodi na wadau wengine wa maendeleo.

Pia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuhakikisha mifumo ya kifedha inakidhi mahitaji ya uchumi wa sasa unaotegemea matumizi makubwa ya teknolojia.

Aidha, matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kuongeza uwazi katika utendaji wa taasisi za umma na kusaidia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa kisasa na shindani.

Amesisitiza kuwa maboresho hayo yataendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuongeza imani ya wananchi pamoja na wawekezaji.