Na. Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeweka mkazo katika utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali vya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti Leo Juni 2,2026 bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Kuwa  vipaumbele hivyo vimeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), pamoja na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi shindani na jumuishi. 

Katika mwaka huo wa fedha, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa sera za fedha na uchumi ili kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji, biashara na uzalishaji yanaendelea kuimarika. Serikali inalenga kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje, sambamba na kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaendelea kuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi.

Kipaumbele kingine ni kuendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma huku ikirahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Aidha, Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Miradi hiyo inahusisha sekta za miundombinu, nishati, maji, afya, elimu na kilimo ambazo zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Katika eneo la usimamizi wa deni la Serikali, Wizara imeweka mkakati wa kuhakikisha mikopo inayoendelea kuchukuliwa inatumika kwenye miradi yenye tija na uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi. Serikali pia itaendelea kuimarisha usimamizi wa hatari za kifedha ili kuhakikisha uthabiti wa uchumi wa taifa unaendelea kuwepo hata katika mazingira ya changamoto za kiuchumi duniani.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo utaendelea kuongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na malengo ya Serikali ya kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi.”.