NA DENIS MLOWE, IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amefungua rasmi Wiki ya Utafiti, Ubunifu na Huduma kwa Jamii inayofanyika kuanzia Juni 2 hadi 4, 2026 katika Viwanja vya Bustani ya Manispaa ya Iringa, akisisitiza umuhimu wa taasisi kushirikiana katika kuonesha huduma zao kwa wananchi kupitia jukwaa moja.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Kheri alisema maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwa na kituo kimoja cha huduma (One Stop Centre) ambapo wananchi wanaweza kupata taarifa na huduma kutoka taasisi mbalimbali kwa wakati mmoja, tofauti na utaratibu wa awali ambapo kila taasisi ilikuwa ikiandaa maonesho yake binafsi.
Alisema mfumo huo mpya utasaidia wananchi kuelewa kwa urahisi huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali huku ukizipa nafasi sawa taasisi kubwa na ndogo kuonesha shughuli na mchango wao katika maendeleo ya jamii.
“Mwananchi anapokuja hapa anakutana na taasisi zote katika eneo moja na kwa wakati mmoja. Hii ni hatua muhimu inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya taasisi mbalimbali,” alisema.
Kheri James aliwataka waandaaji kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa makubwa zaidi mwaka ujao kwa kuwashirikisha wadau wengi zaidi, huku akizihamasisha taasisi ambazo hazikushiriki mwaka huu kujitokeza katika maadhimisho yajayo.
Katika hotuba yake, Kheri alisisitiza nafasi ya utafiti katika kutoa ushauri sahihi kwa viongozi na jamii, akieleza kuwa maamuzi bora yanapaswa kujengwa juu ya matokeo ya tafiti na uchambuzi wa kisayansi.
“Ukipata ushauri sahihi umefanikiwa, lakini ukipata ushauri mbaya unaweza kuharibiwa. Ndiyo maana ni muhimu ushauri unaotolewa uzingatie matokeo ya utafiti ili kusaidia kufanya maamuzi yanayokidhi mahitaji ya wananchi,” alisema.
Aidha, aliwapongeza watafiti na vyuo vikuu kwa mchango wao katika kuibua ubunifu unaolenga kutatua changamoto za jamii alitaja baadhi ya tafiti zilizowasilishwa katika maonesho hayo, ikiwemo matumizi mapya ya zao la ulanzi katika kutengeneza bidhaa za kitabibu na viwandani kwani ubunifu huo unaweza kusaidia kupunguza gharama za vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na kuongeza thamani ya mazao yanayopatikana ndani ya mkoa.
Mkuu wa Mkoa pia aliwashukuru wakuu wa taasisi za umma na binafsi kwa ushiriki wao katika maadhimisho hayo, akisema umoja na uwajibikaji wao umechangia mafanikio ya shughuli mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa mkoani Iringa.
Katika kuonesha dhamira ya Serikali ya Mkoa kuunga mkono maadhimisho hayo, Kheri alitangaza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa shilingi milioni 20 kama mtaji wa kuanzia maandalizi ya maadhimisho ya mwaka 2027.
Alisema lengo ni kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa makubwa zaidi na kuifanya Iringa kuwa kitovu cha utafiti, ubunifu na utoaji wa huduma kwa jamii katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake, RASI wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Profesa Method Samuel Semiono, alisema chuo hicho kimewasilisha miradi mbalimbali ya ubunifu na utafiti inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo mkoani Iringa.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na uzalishaji wa ethanol kutoka ulanzi kwa matumizi mbalimbali, uzalishaji wa uyoga wenye virutubisho maalumu na utafiti wa kemikali za kudhibiti mdudu waharibifu wa zao la nyanya anayefahamika kwa jina la Kantangaze.
Profesa Semiono alisema chuo kimetenga zaidi ya shilingi milioni 300 kusaidia maendeleo ya bunifu hizo na kuzifikisha katika hatua ya uzalishaji wa kibiashara.
Aliwataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi mbalimbali kushirikiana na vyuo vikuu katika kuendeleza bunifu hizo ili ziweze kuleta manufaa kwa jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha taasisi za elimu ya juu, taasisi za utafiti, sekta binafsi na taasisi za umma kwa lengo la kuonesha tafiti, bunifu na huduma mbalimbali zinazochangia maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

