Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, atafanya Ziara ya Kitaifa katika Shirikisho la Urusi kuanzia tarehe 3 hadi 5 Juni 2026, kwa mwaliko wa Rais wa Shirikisho la Urusi, Mheshimiwa Vladimir Putin.

Ziara hii ni ya kihistoria kwa kuwa itakuwa ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Urusi, baada ya ile ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyofanyika mwezi Oktoba mwaka 1969.

Ziara hiyo itaimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.

Wakati wa ziara hiyo, Rais Dkt. Samia atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Putin, katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow. Mazungumzo yao yatajikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati, ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu, sayansi na teknolojia, nishati, madini, kilimo, miundombinu na utalii.

Ziara hiyo inakuja wakati Tanzania ikiendeleza ajenda yake ya diplomasia ya uchumi kupitia ushiriki wake katika majukwaa makubwa ya kimataifa yanayowakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji, taasisi za fedha, sekta binafsi na watunga sera.

Akiwa nchini Urusi, Rais Dkt. Samia atashiriki na kuhutubia katika Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026), ambalo ni miongoni mwa majukwaa yenye ushawishi mkubwa duniani kwa mijadala kuhusu maendeleo ya uchumi, biashara na uwekezaji. Ushiriki wake katika kikao hicho cha ngazi ya juu unaakisi kuongezeka kwa nafasi na ushawishi wa Tanzania katika mijadala ya kimataifa kuhusu uchumi.