Serikali imeandaa mkakati maalum wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ambao umeainisha shughuli mbalimbali zitakazotekelezwa kwa muda mfupi, wa kati na muda mrefu ili kuimarisha sekta ya utoaji haki nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduru, Mhe. Ado Shaibu, katika kikao cha Bunge kinachoendelea Jijini Dodoma Juni 1, 2026 kuhusu mpango wa Serikali wa kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
“Taasisi za Haki Jinai zinaendelea kutoa taarifa za utekelezaji kupitia mfumo wa e-Maboresho ili kuhakikisha uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.” – Mhe. Katimba
Aidha Mhe. Katimba amesema kuwa utekelezaji wa mkakati huo unatekelezwa kupitia wizara za kisekta pamoja na taasisi za Haki Jinai, ambazo zinajumuisha shughuli hizo katika mipango na bajeti zao za kila mwaka.
Ameongeza kuwa Serikali imejenga mfumo wa kielektroniki unaoitwa e-Maboresho, unaotumika kupokea na kufuatilia taarifa za utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa vipindi vya robo mwaka, nusu mwaka na mwaka.
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati huo ili kuhakikisha mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yanatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya sekta ya Sheria na Haki nchini.
