WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumatatu Juni 1, 2026 ameshiriki ibada ya mazishi ya Diwani wa Kata ya Shelui, Mhe. Agnes Nasania, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Shelui, wilayani Iramba mkoani Singida.
Akizungumza katika ibada hiyo, Dkt. Mwigulu amesema marehemu Agnes Nasania alikuwa kiongozi jasiri, mkweli na mwenye msimamo katika kusimamia maslahi ya wananchi wa Kata ya Shelui.
“Agnes alikuwa kiongozi aliyekuwa tayari kusimamia jambo aliloamini ni sahihi kwa manufaa ya wananchi. Alikuwa na ujasiri wa kusema ukweli na kusimamia maendeleo ya watu wake bila kuyumbishwa,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema mchango wa marehemu katika maendeleo ya Kata ya Shelui utaendelea kukumbukwa na wananchi pamoja na viongozi aliowahi kufanya nao kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameahidi kuendelea kuwa karibu na familia ya marehemu na kusaidia ustawi wa watoto wake ili kuhakikisha wanaendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Aidha, amewataka wananchi wa Shelui kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wakati huu wa maombolezo na kuepuka migawanyiko inayoweza kuathiri maendeleo ya eneo hilo.
“Tumpe heshima anayostahili mwenzetu kwa kuendelea kuishi katika umoja na mshikamano alioujenga wakati wa uhai wake. Tusigombane wala kugawanyika katika kipindi hiki cha maombolezo,” amesema.
Awali, akiongoza ibada hiyo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kati (Singida), Dkt. Syprian Hilinti amesema marehemu Agnes Nasania alikuwa kiongozi mwenye moyo wa huduma, aliyewapenda watu na aliyejitolea kwa dhati kulitumikia Kanisa, jamii na taifa.
“Agnes ametuonyesha kuwa inawezekana kuwa mwanasiasa na ukaendelea kuwa mtumishi wa watu, mcha Mungu na mwenye moyo wa kuwahudumia wengine. Alikuwa mtu wa amani, mnyenyekevu na aliyeishi maisha ya kuwatumikia watu,” amesema Askofu Dkt. Hilinti.
Aidha, Askofu Dkt. Hilinti amewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na kuheshimiana bila kujali tofauti za dini, makabila au itikadi, akisisitiza kuwa kipimo cha uongozi ni uwezo wa kutumikia watu na si utambulisho wa mtu.
Marehemu Agnes Nasania alifariki dunia Mei 30, 2026 akiwa Diwani wa Kata ya Shelui katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.

