Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini nchini kuimarisha maadili kwa jamii na kukuza maemdeleo.

Mhr. Sangu amesema hayo alipomwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika hafla ya kumsimika uaskofu mchungaji Daniely Liyaseke wa Kanisa la The Charismatic Episcopal Church of Tanzania, Dayosisi mpya ya Ukanda wa Tanzanite One, iliyofanyika Mei 31, 2026 Kijiji cha Terat, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sangu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa makanisa katika kuimarisha maadili, mshikamano wa kijamii na maendeleo ya Taifa na itaendeleza ushirikiano huo. Ameongeza kuwa kauli mbiu ya kanisa hilo “Kwa neema ya Mungu, tunajenga Huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo” inaakisi dhamira ya kuwekeza kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Vile vile, Mhe. Sangu alisisitiza mambo matatu muhimu kwa Taasisi za dini ziendelee kuombea amani, mshikamano na afya njema kwa viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kadhalika, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na tasasisi za dini katika malezi ya vijana ili kujenga Taifa lenye maadili, upendo na uwajibikaji, pia kuendeleza ushirikiano katika utoaji wa elimu na huduma za kijamii kwa kizazi chenye uzalendo na uwajibikaji.

Aidha, Mhe. Sangu aliongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa, Ofisi na ununuzi wa gari, ambapo katika harambee hiyo Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amechangia Shilingi Milioni 15 na Waziri Sangu amechangia Shilingi Milioni 5.

Naye, Askofu Daniely Liyaseke aliwashukuru viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na waumini kwa mshikamano na ushirikiano, akisisitiza kuwa “ukiona kobe yupo juu ya mti, ujue kuna aliyempandisha.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhe. Fakih Lulandala, walipongeza uongozi wa Askofu Liyaseke na kusisitiza kuwa uwepo wa Dayosisi hiyo ni nguzo ya mshikamano wa kijamii na maendeleo ya kiroho.