Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo ya Serikali ili kuongeza ufanisi katika Utumishi wa Umma.
Akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara na Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mtaa, Juni 1,2026 jijini Dodoma, Waziri Kikwete amesema kuwa viongozi hao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi zinafuatwa katika taasisi zote za umma.
Aidha, Amebainisha kuwa Wakuu wa Rasilimaliwatu ni wawakilishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika maeneo yao ya kazi na wanapaswa kusimamia masuala yote ya kiutumishi kwa weledi, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha mifumo mbalimbali ya kidijitali kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa watumishi wa umma.
Pia ameongeza kuwa viongozi hao wanapaswa kuhakikisha mifumo yote ya kiutumishi inatumika kikamilifu, sambamba na kusimamia haki na stahiki za watumishi kwa wakati ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, amesema kuwa ni wajibu wa Wakuu wa Rasilimaliwatu kushauri waajiri wao kwa usahihi na kuhakikisha watumishi wanapata huduma stahiki kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.
Ameeleza kuwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao utasaidia kujenga Utumishi wa Umma wenye uwajibikaji, uadilifu na matokeo, jambo ambalo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma, matumizi ya teknolojia na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Kikwete amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya viongozi hao kwa lengo la kuhakikisha Utumishi wa Umma unakuwa sikivu, jumuishi na wenye matokeo yanayotarajiwa na wananchi.
Awali akizungumza, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi, amesema kuwa bado kuna changamoto mbalimbali za kiutendaji katika eneo la utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma zinazohitaji kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi wa pamoja.
Amebainisha kuwa kikao kazi hicho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pamoja na kukumbushana masuala muhimu yanayohusu usimamizi wa Utumishi wa Umma.
Aidha, amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa washiriki kujadili changamoto mbalimbali za kiutumishi na kiutawala, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi katika utumishi wa umma.

