Na John Bukuku, Dar es Salaam
Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikishuhudia ukuaji wa uchumi unaoonekana kwenye takwimu za kitaifa, ongezeko la miundombinu, huduma za kijamii na uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, mjadala ulioendelea kuwepo ni iwapo ukuaji huo umefanikiwa kubadilisha maisha ya wananchi wengi kwa kiwango kinachotarajiwa. Hili ndilo eneo ambalo linaonekana kuwa msingi wa tafakuri mpya iliyozaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo sasa inafikia ukomo wake ilifanikiwa kuweka msingi wa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii. Nchi ilishuhudia uwekezaji mkubwa katika barabara, reli, umeme, viwanja vya ndege, elimu na afya. Uchumi ulikua kwa viwango mbalimbali na mazingira ya uwekezaji yaliendelea kuimarika. Hata hivyo, changamoto kubwa iliyobaki ni jinsi ukuaji huo unavyoweza kuonekana moja kwa moja katika maisha ya wananchi na katika uwezo wa uchumi kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa.
Inaonekana serikali imefanya tathmini ya kina kuhusu uzoefu huo kabla ya kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Ndiyo maana katika maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Tume ya Taifa ya Mipango, msisitizo mkubwa umewekwa katika mageuzi ya uwekezaji na uzalishaji kama njia ya kujenga uchumi unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Si jambo la bahati mbaya kwamba kati ya maeneo matatu makubwa ya kimkakati yaliyoidhinishwa na Tume ya Taifa ya Mipango, eneo la mageuzi katika uwekezaji na uzalishaji limepewa viashiria 53 vya upimaji. Hii inaonyesha kuwa serikali imeamua kupima kwa karibu uwezo wa uchumi kuzalisha thamani, ajira na fursa za kipato badala ya kuangalia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla wake.
Kwa muda mrefu Tanzania imeendelea kuuza sehemu kubwa ya malighafi zake zikiwa katika hali ghafi au zikiwa zimeongezewa thamani kidogo. Matokeo yake ni kwamba sehemu kubwa ya faida, ajira na teknolojia imekuwa ikinufaisha nchi zinazofanya uchakataji wa mwisho wa bidhaa hizo. Dira ya 2050 inaonekana kutaka kubadili hali hiyo kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda na uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ndiyo maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Mipango ya taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo wanaonekana kuziangalia kwa umakini wa kipekee sekta za viwanda na ujenzi ambazo zimepewa nafasi maalum katika utekelezaji wa dira hiyo. Kupitia viwanda vya kuongeza thamani, taifa linaweza kunufaika mara mbili; kwanza kwa kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi, na pili kwa kuzalisha ajira nyingi zinazohitajika na vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka.
Msingi wa uchumi jumuishi haujengwi kwa kuongeza pato la taifa pekee, bali kwa kuhakikisha wananchi wengi wanashiriki katika uzalishaji na kunufaika na matokeo yake. Hivyo, kuongeza viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo, madini, mifugo, uvuvi na gesi asilia kunakuwa hatua muhimu ya kuhakikisha faida za rasilimali za taifa zinabaki nchini na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo
Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Mipango kuidhinisha sekta 12 za kipaumbele unaonyesha kuwa serikali imekusudia kujenga mfumo mpana wa uchumi unaounganisha uzalishaji, biashara, teknolojia, elimu na ajira. Hii ni tofauti na mtazamo wa kuangalia sekta moja moja bila kuunganisha mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi.
Sekta ya kilimo ambayo imepewa viashiria 15 vya upimaji inaweza kuwa moja ya maeneo yatakayobeba mafanikio makubwa ya dira hii. Endapo mazao yataongezewa thamani kupitia viwanda vya usindikaji, wakulima wataweza kupata bei nzuri zaidi huku ajira mpya zikizalishwa katika mnyororo mzima wa thamani kuanzia shambani hadi sokoni.
Vivyo hivyo, katika sekta ya madini na nishati, dhamira ya serikali inaonekana kuelekea zaidi kwenye uchimbaji unaoambatana na uchakataji wa ndani ya nchi. Hii ndiyo sababu miradi ya kimkakati kama Mradi wa Nikeli wa Kabanga pamoja na kiwanda cha usafishaji cha Kahama imepewa kipaumbele. Miradi kama hii inaweza kuzalisha ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja huku ikiongeza mapato ya taifa.
Mradi wa Liganga na Mchuchuma nao unaonyesha mwelekeo huo huo. Badala ya kuona madini na makaa ya mawe kama bidhaa za kuuzwa pekee, mradi huo unaweza kuwa kichocheo cha viwanda vya chuma na shughuli nyingine nyingi za uzalishaji zinazotegemea malighafi hizo. Hapo ndipo thamani kubwa ya kiuchumi na ajira inapozalishwa.
Magadi Chumvi Engaruka Monduli mkoani Arusha.
Kadhalika, Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka unaweza kufungua mlango wa viwanda mbalimbali vinavyotumia malighafi hiyo katika uzalishaji. Hii ina maana kwamba manufaa ya mradi hayatabaki katika eneo la uchimbaji pekee, bali yanaweza kuenea katika uchumi mzima kupitia uwekezaji unaotokana na malighafi hiyo.
Mradi wa LNG Lindi unaweza kuwa. mkombozi kwa Watanzania utakapokamilika (Picha mtandao)
Mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) nao ni mfano wa namna serikali inavyotaka kuondoka kwenye uchumi wa kuuza rasilimali ghafi kwenda kwenye uchumi wa kuongeza thamani. Gesi inapochakatwa ndani ya nchi, thamani yake huongezeka zaidi na hutoa fursa nyingi zaidi za ajira, ujuzi na uwekezaji.
Uamuzi wa Rais Samia kuunda mfumo wa usimamizi wa utekelezaji kupitia Delivery Bureau unaonyesha kuwa serikali imejifunza kutokana na changamoto zilizowahi kujitokeza ambapo mipango mizuri ilikuwepo, lakini kasi ya utekelezaji haikufikia matarajio. Safari hii msisitizo umewekwa katika matokeo yanayopimika kupitia viashiria 142 vya mageuzi na viashiria 206 vya sekta za kipaumbele.
Jambo lingine muhimu ni kwamba Dira ya 2050 imeipa nafasi kubwa elimu, sayansi, teknolojia, ubunifu na uchumi wa kidigitali. Hii ni ishara kuwa serikali inatambua kwamba viwanda vya kisasa haviwezi kujengwa bila nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha. Hivyo, ajira zinazolengwa si za kawaida pekee, bali pia ajira za kisasa zinazohitaji maarifa na ubunifu.
Kwa mtazamo mpana, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaonekana kuwa jaribio la kuhamisha mjadala wa maendeleo kutoka katika ukuaji wa uchumi unaopimwa kwa takwimu za kitaifa kwenda katika maendeleo yanayopimwa kwa maisha ya mwananchi mmoja mmoja. Lengo si kuona uchumi unakua pekee, bali kuona wananchi wanapata kazi, kipato na fursa za kushiriki katika uzalishaji.
Machimbo ya Mradi wa Chuma Liganga utakuwa katika kilima hiki kuko Ludewa mkoani Njonbe.
Hatimaye, ikiwa miradi ya kimkakati kama Liganga-Mchuchuma Mkoani Njombe, Engaruka Monduli Arusha, LNG Lindi na Nickel Kabanga Ngara mkoani Kagera itatekelezwa kwa wakati huku sekta za viwanda, kilimo, madini, biashara na teknolojia zikisimamiwa kwa ufanisi, Dira ya 2050 inaweza kuwa hatua muhimu ya kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi wengi zaidi. Hapo ndipo mafanikio ya dira mpya yatakapopimwa; si kwa ukubwa wa uchumi wa taifa pekee, bali kwa idadi ya Watanzania wanaopata ajira, kipato na maisha bora kutokana na ukuaji huo wa uchumi.
Maoni/ Ushauri- 0627869841/ 0713410676
