Na Atley Kuni, WAF-Dar es Salaam 

Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno nchini kupitia uwekezaji wa miundombinu, mafunzo ya wataalamu, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, wakati akifunga rasmi Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Kinywa na Meno Tanzania 2026 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Akifunga maonesha hayo Tayari amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wataalamu, wabunifu, watunga sera, wakufunzi, watengenezaji wa bidhaa za afya ya kinywa na meno, wawekezaji pamoja na wanafunzi kwa lengo la kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.

“Afya ya kinywa na meno ni sehemu muhimu ya afya kwa ujumla na kwamba magonjwa ya kinywa yanaendelea kuathiri mamilioni ya watu duniani kwa kuathiri lishe, elimu, uzalishaji wa kiuchumi, afya ya akili na ustawi wa jamii” amesema Tayari, na kuongeza

“Ushahidi wa kisayansi unaonesha uhusiano mkubwa kati ya magonjwa ya kinywa na meno na magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa, magonjwa ya mapafu, matatizo ya ujauzito na baadhi ya saratani,” amefafanua Tayari.

Naibu Katibu Mkuu ameongeza kuwa, Serikali imepiga hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya afya ikiwemo kupanua hospitali, vituo vya afya na zahanati, kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa na Meno wa mwaka 2026 hadi 2031.

Katika hatua nyingine amesema serikali imeongeza upatikanaji wa wataalamu wa afya ya kinywa na meno, kuboresha miundombinu ya utoaji huduma na kupanua programu za mafunzo huku ikiongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa kinywa na meno.

Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna changamoto zinazokabili sekta hiyo, zikiwemo baadhi ya wananchi kutafuta huduma baada ya maumivu kuwa makali, ongezeko la magonjwa ya fizi na kuoza kwa meno, pamoja na tofauti ya upatikanaji wa huduma kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

“Changamoto zinazotokana na ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe zinahitaji hatua za pamoja kutoka kwa serikali, sekta binafsi, vyama vya kitaaluma na taasisi za elimu,” alisema.

Wakati huo huo, Tayari amesisitiza umuhimu wa matumizi ya vifaa tiba na teknolojia za kisasa zilizosajiliwa na kuthibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na kusema kuwa hakuna mgonjwa anayepaswa kutibiwa kwa kutumia vifaa visivyo na viwango au ambavyo havijaidhinishwa.

Tayari ametumia jukwaa hili kuipongeza TMDA kwa kazi ya kuhakikisha vifaa vya afya vinavyoingia nchini vinasajiliwa, vinapimwa na kufuatiliwa kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa, huku akitoa wito kwa wafanyabiashara na watoa huduma kuendelea kuzingatia matakwa ya kisheria.

Tayari pia alihimiza uwekezaji katika ubunifu wa teknolojia za afya ya kinywa na meno, ikiwemo matumizi ya akili mnemba, uchapishaji wa 3D, tiba kwa njia ya mtandao na mifumo ya kidijitali, akisema Tanzania inahitaji vijana wenye uwezo wa kufanya tafiti na kubuni suluhisho za changamoto za ndani.

Akihitimisha hotuba yake, Tayari amewashukuru waandaaji, wadhamini, waonyeshaji, taasisi za elimu, vyama vya kitaaluma na washiriki wa ndani na nje ya nchi kwa mchango wao wa kufanikisha maonesho hayo.

Takribani nchi 20 kutoka maeneo mbalimbali duniani zimeshiriki kwenye maonesho haya.