Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo amekutana na  Jumuiya ya Diaspora ya Tanzania wanaoishi katika Jamhuri ya Korea na kuwahimiza kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuitangaza nchi na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii. 

Akizungumza katika mkutano uliofanyika  jijini Seoul, Mei 31, 2026,  Balozi Dkt. Kombo alisisitiza umuhimu wa Watanzania wanaoishi nje kuifahamu vizuri nchi wanayoishi, ikiwemo tamaduni zake, lugha, sheria na mifumo ya kijamii ili waweze kujumuika kwa urahisi na kujenga uhusiano chanya unaoweza kuleta manufaa kwa Taifa. 

Alifafanua kuwa uelewa wa mazingira ya nchi mwenyeji huwasaidia diaspora kutambua fursa za kiuchumi na kijamii ambazo zinaweza kuwanufaisha wao pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi husika. 

Pia aliwahimiza kutumia majukwaa yao mbalimbali ya kitaaluma, kijamii na kibiashara kuitangaza Tanzania pamoja na fursa zinazopatikana katika nchi wanazoishi. Alibainisha kuwa kupitia mitandao na ushirikiano wao, diaspora wanayo nafasi kubwa ya kuvutia wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo kuwekeza na kushirikiana na Tanzania. 

Pia alitoa wito kwa Diaspora ambao ni wanafunzi wa elimu ya juu kujikita katika kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali zilizopo nchini hususan katika sekta za afya, maji, elimu na mazingira. 

Kadhalika alitoa rai kwa Diaspora hao kuendelea kudumisha umoja, uzalendo na maadili mema ili kuendeleza taswira chanya ya Tanzania nchini Korea na kimataifa kwa ujumla. 

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya hiyo Bi. Eliusta Filikunjombe alieleza utayari wao wa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutangaza fursa na kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea. 

Awali akizungumza, Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Noel Kaganda alisema idadi ya Diaspora wa Tanzania nchini humo inafikia 300 ambayo inajumuisha wafanyakazi, wafanyabiashara na wanafunzi. 

Mhe. Balozi Dkt Kombo yupo nchini Korea kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Korea na Afrika.