Meneja mahusiano wa Benki ya ushirika Tanzania kanda ya kusini Raphia Mgongolwa,akizungumza jana na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) na Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Mbinga (Mbifacu) mkoani Ruvuma wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo viongozi hao namna ya uendeshaji wa vyama hivyo na matumizi ya mizani za Kidijitali mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mbifacu Mbinga mjini.
Baadhi ya watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)wa wilaya ya Mbinga na Nyasa,wakimsikiliza Meneja Mahusiano wa Benki ya Ushirika nchini Raphia Mgongolwa wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo viongozi hao juu ya matumizi ya mizani za kidijitali zitakazoanza kutumika kupima na kuuza kahawa za wanachama wao msimu wa mauzo 2026/2027.
……….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
Vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na vyama vikuu mkoani Ruvuma, vimehamasishwa kuwekeza kwenye Benki ya ushirika nchini kwa kufungua akaunti au kuwa mawakala ili viweze kuwa sehemu ya wanufaika wa uwekezaji wa benki hiyo kwa ajili ya kupata mitaji ili kuimarisha utendaji wa shughuli zao za ushirika.
Wito huo umetolewa jana na meneja mahusiano wa benki ya ushirika kanda ya kusini Raphia Mgongolwa,wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wa kahawa(Amcos) wilayani Mbinga.
Alisema, benki ya ushirika kwa sasa ipo sokoni na ndiyo benki inayoongoza kutoa huduma bora za kidijitali kwa lengo la kuwafikia watanzania wengi ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa watanzania wakiwemo wakulima mmoja mmoja na wanaojiunga kwenye vyama vya ushirika.
Alisema,wana ushirika wana nguvu kubwa kiuchumi,kwa hiyo kupitia benki ya ushirika wataweza kuimarisha vyama vyao,kukuza uchumi wa mwanachama mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha alisema,wanatoa huduma kwa mkulima mmoja mmoja,Amcos,vyama vikuu na wadau wengine waliopo kwenye mnyororo mzima wa kilimo,wakiwemo wasafirishaji na wauzaji wa pembejeo ambao wana nafasi ya kupata huduma wanazohitaji kwenye benki ya ushirika.
“Sisi benki ya ushirika ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wakulima tumeondoa chagizo la asilimia ishirini,unapohitaji kukopo kwenye benki ya ushirika kama chama haulazimika kuchangiza salio la asilimia ishirini kwa sababu tumeona hiyo ni changamoto kwa vyama vingi vya ushirika kushindwa kupata huduma ”alisema Mgongolwa.
Katika hatua nyingine,Mgongolwa amevitaka vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),vinavyohitaji magari kwa ajili ya usafirishaji katika vyama vyao na kama mradi wa biashara kwenda kufanya biashara na benki hiyo kwani imeweka masharti nafuu ikilinganishwa na benki nyingine hapa nchini.
Amewakaribisha mkulima mmoja mmoja kwenda kukopa mikopo ya kilimo kama pembejeo,trekta na vitendea kazi kwani ni wajibu wa benki hiyo kukuza ushirika na kilimo kwa ujumla kupitia benki ya ushirika hapa nchini.
Pia alisema,benki ya ushirika ina huduma inayojulikana kwa jina la ghala Pesa ambapo mkulima aliyepima mazao na ana stakabadhi(listi) na hajalipwa na chama kikuu au Amcos anaweza kutumia stakabadhi hiyo kukopa fedha hadi asilimia sabini ya fedha anayotarajia kulipwa na chama cha msingi cha ushirika.
Hata hivyo,baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wilayani Mbinga,wameomba benki hiyo kufungua tawi lake Mbinga mjini ili kurahisisha wakulima na wana ushirika kwa ujumla kupata huduma zinazotolewa na benki hiyo.
John Kapinga meneja wa Tingi Amcos alisema,wilaya ya Mbinga na Nyasa ni wazalishaji wakubwa wa kahawa na kuna wakulima wengi waliojiunga kwenye vyama vya msingi vya ushirika,hivyo kukosekana kwa benki hiyo imebabisha wananchama kukimbilia benki nyingine ili kupata huduma hususani za kilimo.
