Mnamo Mei 30, 2026 saa 12:20 asubuhi katika Kijiji cha Mambi, Kata ya Kongolo, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Njombe, Gari yenye namba za usajili T115 DEH ikiwa na Tela namba T150 DFU aina ya Volvo Tank mali ya kampuni ya Syenergy ya Jijini Dar es Salaam ikiwa imebeba shehena ya mafuta aina ya Diesel ikitokea Dar es Salaam kuelekea Mkoa wa Songwe – Tunduma ikiendeshwa na Dereva Mohamed Seif maarufu Maurid [60] mkazi wa Dar es Salaam aliendesha Gari kwa uzembe na kuhama upande wake wa kushoto na kwenda upande wa kulia wa barabara na kuigonga Gari T200 ENQ aina ya Yutong Basi la abiria mali ya kampuni ya ABC Upper Class iliyokuwa inatoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam ikiendeshwa na Dereva aitwaye Ased Asamu maarufu Tembo [40] mkazi wa Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi mmoja na uharibifu wa magari yote mawili.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Ased Asad maarufu Tembo [40] Dereva wa Basi, Letisia Bujabi [32] Kondakta wa Basi na Mohamed Seif maarufu Maurid [60] Dereva wa Lori. Aidha, katika ajali hiyo watu wanne walijeruhiwa kati yao watatu walitibiwa na kuruhusiwa na majeruhi mmoja aitwaye Mariam Abdul [25] mkazi wa Kijichi Dar es Salaam amelazwa katika Hospitali ya Inyala akiendelea kupatiwa matibabu.

Chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva wa Lori kutokuwa makini barabarani akiwa anapishana na Gari lingine.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Imetolewa na:
Kaimu Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.